• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 5:50 AM
JUMA NAMLOLA: Tulitelekeza watoto wetu kwa muda mrefu, sasa tunavuna matunda ya kutojali

JUMA NAMLOLA: Tulitelekeza watoto wetu kwa muda mrefu, sasa tunavuna matunda ya kutojali

Na JUMA NAMLOLA

KINARA wa chama cha ODM, Raila Odinga kwenye kampeni zake miaka iliyopita, alikuwa akisisimua umati kwa hekaya na ngano.

Mojawapo ya ngano hizo, ni hadithi kumhusu ngamia.Bw Odinga alisimulia kuwa siku moja kulikuwa kunanyesha, ngamia akatafuta hifadhi kwenye hema. Kwanza, aliomba aruhusiwe aingize kichwa chake tu ili kisinyeshewe.

Aliporuhusiwa, akaomba aingize na nundu. Alipoingiza nundu akataka aruhusiwe kuingiza na mwili wote. Kwa kuwa hema lilikuwa dogo, lilibomoka na hata mwenye hema akatota. Ingawa hekaya hiyo imekuwa ikitumiwa katika muktadha wa kisiasa pekee, sasa hivi kuna ngamia mpya anayehatarisha kuiweka nchi nzima kwenye mvua na mzizimo kwa muda usiojulikana.

Jumatatu niliwatazama kwa huruma mawaziri Dkt Fred Matiang’i (Usalama wa Ndani) na Profesa George Magoha (Elimu), wakilalama jinsi watoto wamekuwa watukutu na kutaka adhabu ya kiboko irejee shuleni.Kama mwenye ngamia, maafisa hao wakuu serikalini waliruhusu watoto waingize vichwa kwenye hema la nidhamu shuleni.

Wakaingiza nundu na sasa wanaelekea kuingiza mwili mzima.Kama si hivyo, basi ni kwa nini wizara inashindwa kutekeleza Sheria ya Watoto (Iliyorekebishwa 2020)? Kifungu cha 23 C(i) kinawapa wazazi haki ya kuwaongoza na kuwarekebisha watoto kiroho, kitamaduni, kinidhamu na kadhalika.

Tumeruhusu wahuni, wanasiasa, majambazi na waimbaji nyimbo chafu kuwa vielelezo katika jamii. Tumeacha jukumu la jamii nzima kuwa mlezi wa watoto, kwa kusingizia haki za watoto na sasa tunavuna matunda ya kutelekeza majukumu ya ulezi.

You can share this post!

TAHARIRI: Ni hatari kupuuza shida za polisi

Mabwanyenye wa Mt Kenya leo ‘kupitisha’ Raila

T L