• Nairobi
  • Last Updated December 2nd, 2023 1:45 PM
OKA wapendekeza hukumu ya kifo kwa watu wafisadi

OKA wapendekeza hukumu ya kifo kwa watu wafisadi

LUCY MKANYIKA na VALENTINE OBARA

MUUNGANO wa One Kenya Alliance (OKA), umependekeza nchi iweke hukumu ya kifo kwa watu watakaopatikana na hatia ya ufisadi.

Katika ziara yao jana Kaunti ya Taita Taveta, vinara wa muungano huo walirejelea msimamo wao wa kukemea wizi wa mali ya umma.Mwenyekiti wa Chama cha KANU, Bw Gideon Moi, aliambia wananchi, kuwa athari za ufisadi kwa maisha ya raia na taifa zima huwa ni nzito kwa hivyo adhabu ya kosa hilo vile vile inafaa iwe nzito.

Seneta huyo wa Kaunti ya Baringo, alisema OKA ikiunda serikali ijayo, watahakikisha kuna hukumu ya kifo kwa wafisadi ili kukomesha uovu huo nchini.“Wafisadi hakuna haja waende jela. Wale wako na tabia ya ufisadi watabaki na mwili kando, kichwa kando.

Tutachukua hatua kali kwa wale wanaochezea mali ya umma,” akasema.Alikuwa ameandamana na vinara wenzake ambao ni Kiongozi wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, mwenzake wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi, na Seneta wa Bungoma, Bw Moses Wetang’ula anayeongoza Ford-Kenya.

Katika miaka iliyopita, baadhi ya wanasiasa akiwemo Seneta wa Murang’a, Bw Irungu Kang’ata walitoa pendekezo sawa na hilo.Hata hivyo, lilipata pingamizi kutoka kwa wengine wakiwemo viongozi wa mashirika ya kijamii ambao walidai kuwa adhabu hiyo itakiuka haki za binadamu.

Kando na suala hilo, vinara wa OKA walikashifu wapinzani wao wakidai kuwa, hawana uwezo wa kusuluhisha changamoto nyingi zinazokumba Kaunti hiyo hasa kuhusu umiliki wa ardhi na kulinda mapato yanayotokana na uchimbaji wa madini.“Sisi hatuna mashamba hapa.

Kama mtu anasema atatatua mambo ya mashamba na yeye ana mashamba makubwa hapa, atasuluhisha kweli? Tafuteni watu ambao masilahi yao ya kibinafsi hayakinzani na yale ya watu wa Taita Taveta ili wananchi wanufaike,” akasema Bw Mudavadi bila kumtaja yeyote.

Suala la kusuluhisha tatizo kuhusu umiliki wa ardhi Pwani limetumiwa na viongozi wengi wa kisiasa wanaoazimia kuwania urais, akiwemo Naibu Rais William Ruto na Kiongozi wa ODM Raila Odinga.Baina yao, Dkt Ruto ndiye anayefahamika kuendeleza kilimo katika eneo hilo.

Kwa upande wake, Bw Musyoka alisema Naibu Rais anafaa kujiandaa kuondoka mamlakani mwaka ujao.Bw Musyoka alisisitiza kuwa wadau wote wanaohusika katika maandalizi ya uchaguzi ujao wanafaa kuhakikisha uchaguzi utakuwa huru na wa haki.

Naye Bw Wetang’ula aliahidi kuwa, muungano huo ukiunda serikali ijayo, Kaunti ya Taita Taveta itapewa mamlaka ya kusimamia mbuga za wanyama ili pesa ziwafaidi wakazi wa eneo hilo.Kumekuwa na mvutano kati ya serikali ya kaunti na ya kitaifa kuhusu usimamizi wa mbuga ya wanyamapori ya Tsavo.

Jaribio la kaunti kushawishi mahakama iagize serikali ya kitaifa kuikabidhi usimamizi liligonga mwamba, baada ya mahakama kuagiza pande hizo mbili zishauriane na zikubaliane kuhusu suala hilo.

Hata hivyo, serikali ya kaunti imelalamika kuwa serikali ya kitaifa haijajitolea kutimiza mashauriano yaliyoagizwa.

You can share this post!

Viongozi wasutwa kukosa kikao cha Jumuia ya Pwani

TAHARIRI: Ni hatari kupuuza shida za polisi

T L