• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 3:31 PM
TAHARIRI: Njaa: Wanafunzi katika maeneo kame walishwe shuleni hata wakati wa likizo

TAHARIRI: Njaa: Wanafunzi katika maeneo kame walishwe shuleni hata wakati wa likizo

NA MHARIRI

HATUA ya kituo cha Mukuru Promotion Centre (MPC) kuendelea kuwapa wanafunzi wa mtaa wa Mukuru, Nairobi, chakula cha bure hata wakati wa likizo, inafaa kupongezwa.

Kwa mujibu wa usimamizi wa kituo cha MPC, wanafunzi watakuwa wanapewa chakula mara mbili – asubuhi na mchana – hadi pale shule zitakapofunguliwa Januari, mwaka ujao.

Hatua hiyo itasaidia pakubwa kuhakikisha kwamba wanafunzi wa mtaa huo wa mabanda wanajiepusha na visa vya uhalifu au kugeuka ombaomba ili kupata chakula cha kutia tumboni wakati wa likizo.

Mpango huo wa kulisha wanafunzi kutoka familia maskini wakati wa likizo unafaa kuigwa na serikali pamoja na mashirika mengineyo ya wahisani.

Serikali pamoja na mashirika mbalimbali yamekuwa yakilisha wanafunzi shuleni katika kaunti mbalimbali nchini kwa lengo la kuhakikisha kuwa watoto wanasoma bila kuhangaishwa na makali ya njaa. Lakini mpango huo wa lishe shuleni hukoma shule zinapofungwa na kuwaacha watoto hao kuhangaika wakiwa nyumbani.

Serikali imekuwa ikilisha zaidi ya wanafunzi 2.5 milioni, haswa katika maeneo kame na mitaa ya mabanda.

Katika manifesto ya Kenya Kwanza, Rais William Ruto ameahidi kuongeza maradufu idadi ya wanafunzi wanaopata chakula cha bure shuleni.

Serikali ilijitwika jukumu la kulisha wanafunzi shuleni katika maeneo kame mnamo 2018 ilipokabidhiwa na Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP).

Ripoti mbalimbali zimeonyesha kuwa chakula cha bure shuleni kimechangia pakubwa katika matokeo bora na kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaojiunga na masomo.

Wakenya zaidi ya milioni 4, wengi wao wakiwa watoto, sasa wanahitaji chakula cha msaada kwa haraka ili kuwanusuru kutokana na makali ya njaa.

Takwimu za serikali zinaonyesha kuwa watoto milioni 1 katika kaunti 14; zikiwemo Laikipia, Marsabit, Garissa, Isiolo, Samburu, Tana River, Turkana, Wajir na Mandera, tayari wanaugua utapiamlo kutokana na ukosefu wa chakula.

Hatua ya serikali, kupitia kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, kuwasihi Wakenya wanaofanya kazi kutoa sehemu ya mishahara yao kusaidia waathiriwa wa njaa ni ishara kuwa hali ni mbaya nchini.

Ukweli ni kwamba chakula cha msaada ambacho kimekuwa kikitolewa na serikali hakitoshi.

Hivyo basi, kuna haja kwa serikali kuendeleza mpango wa kulisha wanafunzi shuleni hata wakati wa likizo.

Hatua hiyo itawaletea afueni wazazi ambao wamekuwa wakihangaika kulisha watoto wao.

Mpango huo utalinda watoto katika maeneo kame na mitaa ya mabanda dhidi ya maradhi ya utapiamlo.

Vilevile, chakula shuleni wakati wa likizo kitasaidia watoto katika maeneo kame na mitaa ya mabanda kutojihusisha na vitendo vya uhalifu.

Kuna haja ya wabunge kubuni sheria itakayohakikisha kuwa wanafunzi wanaonufaika na chakula cha bure shuleni wanaendelea kupewa hata wakati wa likizo.

  • Tags

You can share this post!

MWALIMU WA WIKI: Mbunifu, mtafiti na mwajibikaji pia

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Ujerumani na Uhispania nguvu sawa...

T L