• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 10:55 AM
TAHARIRI: Raila ajifunze kudumisha washirika wake kisiasa

TAHARIRI: Raila ajifunze kudumisha washirika wake kisiasa

NA MHARIRI

BW Odinga ni kiongozi mjanja anayejua kucheza karata zake kisiasa kwa weledi mkuu.

Ila amefeli kujifunza kutokana na makosa ya kushindwa kudumisha washirika wake kisiasa na kutovumilia wakosoaji chamani.

Baada ya kutangaza kuwa hatambui utawala wa Rais William Ruto, wabunge watano wa ODM – akiwemo chipukizi wa Lang’ata, Bw Felix Odiwuor ‘Jalango’ – walimkaidi na kukutana na Dkt Ruto katika Ikulu ya Nairobi.

Walidai walikuwa wakifuatilia maendeleo katika maeneo yao ya uwakilishi, kitendo kilichomuudhi Bw Odinga na ODM kwa jumla.Kikatiba maeneo yote nchini yanafaa kupata maendeleo kwa usawa bila kujali ikiwa mbunge wao ametembelea Rais au la.

Hivyo, huenda walipotoshwa au walifanya hivyo kwa sababu zao binafsi.Ingawa hivyo, ODM ithibitishe haki na usawa kwa kuwapa nafasi kujieleza.

Naye Bw Odinga afahamu kuwa hii ni fursa ya kujenga uhusiano thabiti na wabunge vijana hasa wanaoonekana kuwa na maoni kinzani, ili kujua kiini cha uasi wao chamani.

Haikuwa busara kwa chama kumfurusha Jalang’o katika kikao cha Azimio majuzi.

Japo kina uwezo wa kuadhibu waasi, kitakosea kuanza mchakato wa kuwatimua badala ya kushauriana nao ili kukuza umoja na uhuru wa demokrasia katika ODM.

Ikiwa tutakosa vyama imara nje na ndani ya Bunge, kama ODM, tutasambaratisha juhudi za ukombozi, na kuacha serikali yenye mamlaka kufinya zaidi walipaushuru.Kwa vile Bw Odinga ndiye shujaa katika safari hii ya ukombozi anafaa kuonyesha moyo wa kusamehe na kukumbatia maoni tofauti. La sivyo, atawapa mahasimu wake makombora ya kumshambulia yeye na ODM.

  • Tags

You can share this post!

JAMVI LA SIASA: ‘Jeshi’ la Uhuru lililobaki...

Kamanda wa polisi hatarini kufurusha familia 100

T L