• Nairobi
  • Last Updated May 22nd, 2024 6:07 PM
TAHARIRI: Serikali ianze upesi ujenzi wa mabwawa 200 iliyoahidi

TAHARIRI: Serikali ianze upesi ujenzi wa mabwawa 200 iliyoahidi

NA MHARIRI

HUKU Kenya ikiendelea kukabiliana na njaa kali na ukame uliokithiri, mjadala kuhusu jukumu la mabwawa makubwa katika kutatua changamoto hizi ni muhimu mno.

Lakini awali ya yote, japo serikali ya Kenya Kwanza chini ya Rais William Ruto imeeleza mpango wake wa kujenga zaidi ya mabwawa 200 makubwa kote nchini, tunaamini kuwa Kenya inahitaji zaidi ya idadi hiyo ili kutokomeza kabisa shida ya uhaba wa chakula na ukame.

Kwanza, ujenzi wa mabwawa hayo utaimarisha kilimo cha unyunyiziaji, ambacho ni muhimu kwa utoshelevu wa chakula.

Huku zaidi ya asilimia 80 ya ardhi ya Kenya ikiwa katika maeneo yenye ukame na kiangazi, kilimo cha unyunyiziaji ndicho njia pekee ya kuzidisha uzalishaji wa mazao na kuhakikisha lishe na chakula cha kutosha kinapatikana.

Ujenzi wa mabwawa hayo utakuwa hakikisho tosha la upatikanaji wa maji ya kilimo cha unyunyiziaji, hasa katika misimu ya kiangazi.

Mbali na kupiga jeki uzalishaji wa chakula, hatua hiyo pia itabuni fursa za ajira kwa maelfu ya Wakenya.

Pili, mabwawa makubwa ni njia ya hakika ya kuhifadhi maji, ambayo ni rasilimali adimu nchini Kenya. Kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa (tabianchi) yanayozidi kusababisha ukame wa muda mrefu, ni bora mbinu za kuhifadhi maji ya mvua zibuniwe.

Kenya ikiteka na kuyahifadhi maji ya mvua katika misimu ya mvua nyingi, yanaweza kutumika wakati wa kiangazi. Hilo likifanikishwa, wakulima watasaidiwa kupunguza utegemezi zaidi wa maji ya mvua kwa kilimo chao.

Aidha, ujenzi wa mabwawa hayo utaimarisha uzalishaji wa kawi au nguvu za umeme, ambao ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi.

Ukuaji wa uchumi wa Kenya unategemea pakubwa upatikanaji mzuri wa nguvu za umeme wenye bei nafuu.

Huku idadi ya watu nchini ikitarajiwa kuongezeka maradufu katika miaka 25 ijayo, kutakuwa na ongezeko la mahitaji ya nguvu hizo.

Ujenzi wa mabwawa makubwa utawezesha upatikanaji wa kawi hiyo kwa wingi ambayo itafaulisha maendeleo ya viwanda na kuunda nafasi za kazi hasa kwa vijana wetu.

Maadamu msafiri ni aliye bandarini, tunaunga mkono kwa dhati mpango wa serikali ya Kenya kuanza ujenzi wa mabwawa hayo 200 kabla ya kuwazia kuongeza mengine zaidi; yaani safari ndefu huanza kwa hatua moja.

Hata hivyo, itakuwa muhimu kuhakikisha kwamba ujenzi huo unafanywa haraka na kwa njia endelevu, kwa kuzingatia athari za kijamii na mazingira.

Serikali pia iwashirikishe wanajamii katika mchakato wa kufanya maamuzi na kuhakikisha wananufaika na mradi huo.

  • Tags

You can share this post!

Zaidi ya maafisa 3 wauawa na kilipuzi

NTSA yatayarisha sheria ya kudhibiti sekta ya bodaboda

T L