• Nairobi
  • Last Updated May 14th, 2024 5:55 AM
Zaidi ya maafisa 3 wauawa na kilipuzi

Zaidi ya maafisa 3 wauawa na kilipuzi

NA MANASE OTSIALO

MAAFISA wa polisi wasiopungua watatu kutoka Kitengo cha Doria Mpakani (BPU) waliuawa jana wakati gari walilokuwa wakisafiria lilipolipuliwa.

Kundi hilo la maafisa wanne lilikuwa likielekea Garissa kutoka kambi yao ya Kulan kabla ya mkasa huo.

“Tukio hilo lilitendeka kwenye barabara kuu ya Garissa-Dadaab –Liboi ambapo gari la walinda usalama lilikumbana na kilipuzi kilichotegwa barabarani. Tulipoteza maafisa watatu huku wa nne akijeruhwa vibaya,” alisema Naibu Kamishna wa kaunti ndogo ya Dadaab, Kipkirui Siele.

Kulingana na DCC, kilipuzi hicho kiliwalenga maafisa wa polisi waliokuwa wakitumia barabara hiyo.

“Tunashuku kuna mtu aliyelipua kilipuzi hicho mara tu gari hilo lilipowasili. Hii ni barabara yenye shughuli nyingi na magari mengine mengi yalikuwa yamepita bila matatizo yoyote hadi hili lilipofika,” alisema.

Alisisitiza kuwa kilipuzi hicho kilikuwa kinadhibitiwa kwa kutumia kifaa maalum.

Hii si mara ya kwanza barabara hiyo ya Garissa-Dadaab-Liboi imekumbwa na visa vya vilipuzi.

Mnamo Julai 29, 2022, wataalam wa vilipuzi kutoka kambi ya Liboi walitegua vifaa viwili vilivyokuwa vimetegwa kwenye barabara ya Dadaab-Kulan-Liboi.

Maafisa katika Kituo cha Polisi cha Liboi waliarifiwa na mchungaji mifugo kuhusu nyaya mbili zilizojitokeza ardhini kwenye barabara hiyo.

Vikosi vya polisi na wanajeshi viligundua kuwa angalau vilipuzi viwili (IEDs) vilikuwa vimetegwa katikati ya barabara eneo hilo.

Naibu spika wa zamani katika Bunge la Kitaifa ambaye sasa ni Mbunge wa Dadaab, Farah Maalim, aliyekuwa kwenye msafara wa kampeni alidai kupitia kurasa zake kwenye mitandao ya kijamii kwamba ndiye aliyekuwa akilengwa.

Mnamo Januari mwaka huo huo, maafisa wanne wa polisi waliuawa wakati gari walilokuwa wakisafiria liliposhambuliwa na wavamizi waliojihami kwa bunduki kwenye barabara hiyo.

Maafisa hao walikuwa wakisafiri kwa kutumia gari aina ya probox waliposhambuliwa kwenye eneo lililopo kati ya Liboi na Kulan.

Mashahidi walisema walisikia milio ya bunduki kutoka eneo la Damajale na walipokwenda kutazama wakapata miili ya maafisa hao wanne hapo.

Maafisa hao walipokonywa bunduki zao tatu aina ya AK47 na idadi isiyojulikana ya risasi.

Kisa kibaya zaidi kutendeka kwenye barabara hiyo hiyo kilirekodiwa mnamo Oktoba 2019 wakati maafisa 11 wa kulinda usalama kutoka Kitengo cha GSU waliuawa kwenye mlipuko mbaya baada ya gari lao kupitia juu ya kilipuzi.

  • Tags

You can share this post!

BENSON MATHEKA: Ni hatari kuu Bunge kupoteza uhuru wake wa...

TAHARIRI: Serikali ianze upesi ujenzi wa mabwawa 200...

T L