• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
TAHARIRI: Serikali iseme ukweli kuhusu kuvuja mtihani unaoendelea

TAHARIRI: Serikali iseme ukweli kuhusu kuvuja mtihani unaoendelea

NA MHARIRI

IDARA ya Upelelezi wa Jinai (DCI) inawazuilia watu walio kwenye genge linalosambaza karatasi za mtihani wa kitaifa wa kidato cha Nne (KCSE).

DCI imefichua kuwa karatasi hizo zimekuwa zikisambazwa kupitia makundi ya WhatsApp, na kwamba wanafunzi au wazazi wao wamekuwa wakitoa kati ya Sh500 na Sh2,000 kwa kila karatasi.

Ufichuzi huu unajiri wakati ambapo serikali kupitia waziri wa Elimu George Magoha, imekuwa ikikana kuwepo kwa jambo kama hilo.

Profesa Magoha amekuwa akitumia kimombo kingi na kusema ‘kuonekana mapema kwa karatasi, si wizi wa mtihani.’

Kimombo hiki kwa lugha nyepesi kuwa watu wanaobahatika kuuona mtihani kabla ya wakati wake, hawawazidi wenzao wanaosubiri hadi muda wa mtihani ufike.

Kauli kama hii kutoka kwa mtu mwenye elimu ya kiwango cha uprofesa, inaonyesha ni kiasi gani serikali haiko tayari kukiri makosa yanapotokea.

Wanafunzi wanaobahatika kuuona mtihani kupitia WhatsApp kabla ya wenzao, bila shaka watajiandaa na majibu sahihi kabla ya kuingia ndani ya chumba cha mtihani.

Ni wiki jana tu ambapo ufunguo wa kasha la kuhifadhia mitihani mjini Eldoret ulisemekana kupotea.

Serikali haijasema hadharani kama ilibadilisha kufuli za kasha hilo au la.

Wakenya wataamini vipi kuwa kisa hicho hakikuwa sehemu ya njama za watu wenye uchu wa pesa, kuwa na nafasi ya kuiba mtihani ili wausambaze kwa walio tayari kuununua?

Wizi huu unaoendelezwa kwa walio na uwezo wa kununua ni hatari kwa nchi yetu. Mtoto wa tajiri anapoiba mtihani kisha apate alama za kujiunga na Chuo Kikuu, huko pia ataendeleza tabia hii.

Iwapo atakuwa daktari, tuna uhakika gani kuwa atawapa wagonjwa tiba inayostahili?

Akiwa mhandisi wa ujenzi, tutaendelea kuona majumba yakiporomoka.

Ingawa serikali inaendelea kukanusha kuvuja kwa mitihani, kukamatwa kwa washukiwa kwafaa kuwa mwanzo wa upelekezi wa kina.

Ni lazima DCI ituambie ni akina nani hao wanaoweza kuifungua mitihani na kuipiga picha, kisha wakaifunga bila mtu kugundua.

Kama ni kweli kuwa mitihani hulindwa na maafisa wa polisi saa 24, je, kuna uwezekano kuwa polisi hushirikiana na wahalifu kuuza mitihani ili wapewe kitu kidogo

Maswali haya ni muhimu sasa hivi. Mtihani haufanywi tu kwa lengo la kupita, bali kufahamu ni kiwango gani cha maarifa mwanafunzi huwa amepata kwa miaka aliyokuwa shuleni.

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Munya asije akasahau Kiunjuri aliwezesha...

Bunge la kaunti latoa msaada kwa shule ya umma

T L