• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
TAHARIRI: Serikali iwape wakimbizi wa Mau makazi

TAHARIRI: Serikali iwape wakimbizi wa Mau makazi

Na MHARIRI

JUMA hili kumeripotiwa habari za kutamausha sana kuhusu visa na masaibu yanayowakumba watu waliofurushwa na serikali kuu kutoka msitu wa Mau.

Imeripotiwa kwamba wanaume wanapigana na hata kuuana kutokana na visa vya ubakaji katika kambi hizi za wakimbizi wa ndani kwa ndani.

Kwa mujibu wa Katiba ya Kenya, ni haki kwa kila mwananchi kupata makazi na chakula kwani haya ni mahitaji ya kimsingi kwa binadamu yeyote.

Hitaji hili la kikatiba linatoa takwa hili kwa ufahamu kwamba binadamu si mnyama wa porini na hivyo basi anafaa kupewa heshima anayostahili.

Kuna uwezekano kwamba viongozi wanaohusika wamekosa kutekeleza jukumu lao labda kutokana na mtazamo kwamba wakimbizi hawa walinyakua mashamba katika msitu wa serikali na hivyo basi hakuna haja ya kufidia ‘wavamizi.’

Hata hivyo, ni muhimu ikumbukwe kwambaa katika msururu wa visa vya unyakuzi wa mashamba ya misitu nchini, wahusika wakuu huwa wanasiasa na viongozi wenye ushawishi mkubwa katika serikali.

Viongozi hawa hunyakua mashamba ya serikali, kutafuta hati ghushi kwa ardhi hizi kisha huuzia watu maskini wasiokuwa na habari.

Serikali ijapo, ni maskini waliokamua jasho lao kununua vipande hivi vya ardhi ndio ambao huonekana wakosaji na kuadhibiwa kutokana na makosa ya ‘wakubwa’ serikalini.

Juma hili kumeripotiwa visa vya wanaume kuuana kutokana na hatua ya baadhi yao kuwania wanawake katika kambi hizi za wakimbizi mlimani Mau.

Yapo madai ya kuwepo baadhi ya wanaume ambao wanawavizia wanawake wasio na habari katika makazi haya duni na kuwabaka au kuwashawishi washiriki ngono kutokana na madhila wanayopitia.

Visa hivi vigunduliwapo, wahusika husakwa na kuuawa na wanaume wenzao kama njia ya kulipiza kisasi.Visa hivi vya mauaji katika kambi za wakimbizi vinakuwa tu kama kugonga msumari moto kwenye kidonda.

Hatufai kuwa na taifa ambapo serikali inaona madhila wanayopitia raia wake kisha haichukui hatua yoyote. Huu ni unyama kwani baadhi ya maovu yanayoendelea katika kambi hizi hayatokei kwa kupenda.

Serikali inafaa ichue hatua kusuluhisha visa vya Wakenya kugeuzwa kuwa wakimbizi katika nchi yao.

Mabwanyenye wanaonyakua mashamba kisha kuwauzia maskini wanafaa kusakwa na kushtakiwa kama njia mojawapo ya kukomesha ufisadi na matumizi mabaya ya nafasi za uongozi.

Na maadamu kosa halipaswi kusuluhishwa kwa kosa jingine, serikali inafaa kutafutia wakimbizi hawa makazi na ardhi mbadala kisha iwasake wanyakuzi wa ardhi.

You can share this post!

Mbunge alaani hatua ya wakazi kuweka uchawi mbele kuliko...

AFCON: Senegal wakomoa Cape Verde na kuingia robo-fainali

T L