• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
AFCON: Senegal wakomoa Cape Verde na kuingia robo-fainali

AFCON: Senegal wakomoa Cape Verde na kuingia robo-fainali

Na MASHIRIKA

FOWADI Sadio Mane alifungulia Senegal ukurasa wa mabao katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Cape Verde mnamo Jumanne usiku na kufuzu kwa robo-fainali ambayo sasa itawakutanisha na mshindi wa mechi kati ya Mali na Equatorial Guinea.

Mane alicheka na nyavu za wapinzani wao dakika chache baada ya kipa wa Cape Verde, Vozinha, kuonyeshwa kadi nyekundu kwa hatia ya kumkabili visivyo fowadi huyo wa Liverpool.

Licha ya kuumia na kupoteza fahamu kwa muda mfupi baada ya kukabiliwa na Vozinha, Mane alinyanyuka na kuendelea na mchezo. Baada ya kufunga bao, aliomba kuondolewa uwanjani na akapelekwa hospitalini kwa matibabu zaidi.

Kuondolewa kwa Vozinha kulisaza Cape Verde na wachezaji tisa pekee uwanjani kwa kuwa kiungo Patrick Andrade alikuwa tayari amefurushwa katika dakika ya 21. Bao la pili la Senegal lilijazwa kimiani na Bamba Dieng mwishoni mwa kipindi cha pili.

Japo Senegal hawakuridhisha katika raundi ya makundi, ni miongoni mwa vikosi vinavyopigiwa upatu wa kutawazwa wafalme mwaka huu ikizingatiwa uthabiti wa kikosi chao kinachojivunia huduma za Idrissa Gueye (PSG), Mane (Liverpool), Edouard Mendy (Chelsea), Abdou Diallo (PSG) na Kalidou Koulibaly (Napoli).

Wanafainali hao wa AFCON 2002 na 2019, walielekea Cameroon baada ya kujizolea alama 14 kutokana na mechi sita za hatua ya mchujo. Hata hivyo, walifungua kampeni za Kundi B jijini Yaounde kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Zimbabwe kisha kuambulia sare tasa dhidi ya Guinea na Malawi.

Matokeo hayo yaliwaweka kileleni mwa Kundi B kwa alama tano, moja nyuma ya Guinea na Malawi waliopigwa na Guinea 1-0 kabla ya kushinda Zimbabwe 2-1 na kutoshana nguvu na Senegal.

Senegal wanaoshikilia nafasi ya kwanza barani Afrika, ndicho kikosi kinachojivunia kufuzu kwa fainali za AFCON mara nyingi zaidi bila kunyanyua taji. Masogora hao wa walizidiwa ujanja na Cameroon kupitia penalti kwenye fainali ya 2002 nchini Mali kabla ya Algeria kuwakomoa 1-0 mnamo 2019 nchini Misri.

Licha ya kusuasua, Senegal ndicho kikosi cha pekee ambacho hakijafungwa bao kufikia sasa kwenye makala ya 33 ya AFCON mwaka huu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

TAHARIRI: Serikali iwape wakimbizi wa Mau makazi

Maseneta walalamikia kuzimwa kuenda mataifa ya kigeni

T L