• Nairobi
  • Last Updated February 26th, 2024 10:25 AM
TAHARIRI: Serikali yafaa ieleze iwapo mahindi ya kuagizwa ni ya GMO au la

TAHARIRI: Serikali yafaa ieleze iwapo mahindi ya kuagizwa ni ya GMO au la

NA MHARIRI

SERIKALI imetangaza kuwa mahindi ya bei nafuu yanaingia nchini kuanzia leo Jumatano ili kuziba pengo la uhaba wa mlo huo.

Kutokana na hatua hiyo, wakulima wa mahindi hasa katika eneo la North Rift wameanza kulalamika kuwa watapata hasara kubwa iwapo watauza mahindi yao kwa bei ya chini baada ya mahindi ya bei rahisi kutoka nje ya nchi kuingizwa nchini.

Ingawa sababu ambayo serikali ilitoa ina mashiko, uagizaji wa bidhaa hiyo kabla ya mahindi ya wakulima kununuliwa hadi kwisha unawavunja moyo wakulima hao.

Inapozingatiwa kuwa pembejeo zilizotumika kuzalisha mahindi hayo zilinunuliwa kwa bei ghali, serikali ingetafuta mbinu mwafaka ya kuwalinda dhidi ya bei ya chini watakayolazimika kuuza zao lao kutokana na ushindani ujao.

Huenda wengi wao wakaamua kususia kilimo hicho katika siku zijazo na hivyo basi kusababisha uhaba wake.

Zaidi ya hayo, serikali haijawafafanulia Wakenya iwapo mahindi hayo yanayoagizwa ni yaliyobadilishwa vinasaba kisayansi (GMO) au la.

Mwishoni mwa mwaka 2022, waziri wa Biashara na Viwanda, Bw Moses Kuria alisema serikali ilinuia kuagiza mahindi ya GMO magunia milioni 10. Baada ya malalamiko ya Wakenya, serikali ilipiga breki mpango huo.

Suala la GMO liliibua mihemko iliyoashiria kuwa Wakenya bado hawako tayari kukumbatia mazao au bidhaa zilizofanyiwa ukarabati wa kisayansi.

Baada ya serikali kunyamaza kwa miezi mitatu ilipositisha uagizaji wa mahindi ya GMO, iliibuka na kutangaza kuwa mahindi magunia milioni 10 yataanza kuwasili nchini mwezi huu wa Februari. Lakini haikufafanua iwapo mahindi hayo yalikuwa ya GMO au la.

Sintofahamu hiyo inaibua hofu kuwa huenda serikali inataka kuwalazimisha Wakenya kula chakula cha GMO.

Hofu hiyo inatiliwa nguvu na matamshi ya Rais William Ruto, akihojiwa na wanahabari wa runinga za Kenya, kuwa GMO haina madhara yoyote kwa binadamu.

Kwa namna fulani msimamo wake huo ulifasiriwa kama unaounga mkono chakula cha GMO. Katika nchi zilizoendelea, bidhaa za GMO hutiwa nembo ya kuzibainisha.

  • Tags

You can share this post!

Mabingwa wa insha Pwani wapimana ujuzi

CECIL ODONGO: Ibada zisigeuzwe jukwaa la kutupiana cheche...

T L