• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
CECIL ODONGO: Ibada zisigeuzwe jukwaa la kutupiana cheche za kisiasa

CECIL ODONGO: Ibada zisigeuzwe jukwaa la kutupiana cheche za kisiasa

NA CECIL ODONGO

RAIS William Ruto na viongozi wa Kenya Kwanza wakome kuhadaa Wakenya kwamba mikutano wanayoandaa katika kaunti mbalimbali kila Jumapili ni ya maombi, ilhali ni ya kumpiga vita Raila Odinga.

Tangu washinde uchaguzi, Rais Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua pamoja na viongozi wa Kenya Kwanza (KK) wamehudhuria ibada za pamoja zinazoshirikisha makanisa mbalimbali.

Baadhi ya kaunti ambazo wamehudhuria ibada hizo ni Homa Bay, Bomet, Uasin Gishu, Kitui, Trans Nzoia, Embu, Kirinyaga, na Narok.

Hata hivyo, kinachojitokeza zaidi ni kuwa majukwaa takatifu kanisani sasa yanatumika kumkemea Bw Odinga, ambaye ameanza kuchochea maasi ya umma dhidi ya serikali.

Kwanini mikutano hii hutangazwa kama ibada za shukrani ilhali kwa kiasi kikubwa inatawaliwa na kejeli na za hamaki?

Mbona viongozi wasiandae hafla zao za kisiasa badala ya kujificha nyuma ya pazia la dini kisha kumtafuta maneno kinara huyo wa upinzani?

Wikendi iliyopita akiwa Kaunti ya Narok, Rais Ruto mwenyewe alimshambulia Bw Odinga kwa maneno makali akisema hadhara za kinara huyo wa upinzani ni za kushinikiza amuingize serikalini.

Hii ni licha ya kinara huyo kukariri mara kadhaa kwamba hataki hata robo ya utawala wa KK.

Katika ibada hiyo, Bw Gachagua alimsuta Waziri Mkuu huyo wa zamani kama kiongozi msumbufu ambaye aliiga usumbufu ambao babake marehemu Jaramogi Oginga Odinga alimtatiza nao Mzee Jomo Kenyatta.

Bw Gachagua ameingiwa na sahau kwani marehemu Oginga alipigania uhuru tulionao kwa sasa na kumkweza Mzee Kenyatta hadi akawa Rais.

Pia Naibu Rais alifumbia macho hoja kwamba Raila alikuwa mstari wa mbele kupigania ukombozi wa pili na katiba mpya ambayo inatumika kwa sasa.

Matamshi hayo yalitolewa wakati wa ibada. Cha kushangaza ni kuwa, baadhi ya viongozi walipiga makofi na kushangilia.

Hata viongozi wa makanisa ni kana kwamba wamekuwa na miegemeo ya kisiasa, walikuwa kimya cheche hizo kali za kisiasa zikipigwa madhabahuni.

Haifai kiongozi wa dini kumpigia mwanasiasa makofi kwa kumtusi au kumdhalilisha mtu, tena wakati wa ibada.

Viongozi wa dini waige waliokuwa maaskofu Alexander Kipsang Muge, Henry Okullu, Ndingi Mwana Nzeki, David Gitari, na Manasses Kuria ambao walikuwa na ujasiri kupinga utawala dhalimu wa marehemu Rais Daniel Arap Moi.

Iwapo wataendelea kuwapigia makofi wanasiasa wanaoporomosha matusi wakitumia majukwaa ya makanisa, basi watageuka watumwa wa utawala uliopo.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Serikali yafaa ieleze iwapo mahindi ya kuagizwa...

CHARLES WASONGA: Serikali iwachukulie hatua kali walimu...

T L