• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:12 PM
TAHARIRI: Uadilifu ndiyo chanjo ya siasa chafu za Kenya

TAHARIRI: Uadilifu ndiyo chanjo ya siasa chafu za Kenya

NA MHARIRI

SIASA katika yaliyoendelea hasa Ulaya huongozwa na sera madhubuti.

Siasa za namna hii zimechangia kuimarisha na kupevusha demokrasia ya mataifa haya kiasi kwamba michakato ya kisiasa ni bainifu na huwa haikumbwi na misukosuko.

Uthabiti na ustawi unaopatikana katika mataifa haya pakubwa umechangiwa na utulivu wa kisiasa unaoshuhudiwa katika nchi husika. Katika mataifa ya hadhi hii, siasa si suala la kufa kupona kama ilivyo katika mataifa ya ulimwengu wa tatu.

Katika mataifa mengi ya Afrika ambayo aghalabu yana misingi hafifu ya demokrasia, siasa zinaendeshwa kwa misingi ya hadaa na inda kubwa ya tabaka tawala.

Ni hadaa hii ambayo pamoja na ubinafsi hutumbukiza mataifa mengi ya Afrika katika ghasia za baada ya uchaguzi.

Ni katika bara letu ambapo wanasiasa hutoa ahadi ambayo wao wenyewe wanafahamu fika kwamba haziwezi kutimizwa. Ahadi hizi hutolewa tu ili kuwapa raia matumaini.

Mihula ya uongozi ikaribiapo mwisho, wanasiasa wawa hawa hurejea bila soni kutoa ahadi hewa mpya. Subira ya wananchi ifikiapo kilele, matumaini hugeuka kuwa hasira.

Hasira na kukata tamaa huku ndiko kumejaa katika nyoyo za wapigakura wengi. Kila uchaguzi ufikapo watu wengi hawaoni haja ya kushiriki katika zoezi hili.

Umefika wakati ambapo wananchi wanafaa kuanza kuwawajibisha wanasiasa kwa kukataa hadaa zao. Mingi ya miungano ya kisiasa kwa muda mrefu imekuwa ikiundwa na makundi ya watu wenye maslahi binafsi wanaoafikiana kuja pamoja kuwafyonza raia.

Udhaifu wetu raia ambao wanasiasa wanaujua na hupenda kuutumia kila wakati wa uchaguzi ni ukabila.

Wanajua kwamba ukiwagonganisha watu kwa msingi wa kikabila itakuwa rahisi kuwatenga katika makundi kisha uungwaji mkono wao utumike kwa maslahi binafsi kuwafaidi wao.

Ni kutokana na sifa hizi za wanasiasa wetu ambapo wananchi wote hasa katika taifa letu wanafaa kuungana na kung’amua kwamba hali ya maisha inapozorota, ni wao ndio huumia.

Tabaka la viongozi wawe katika serikali au katika upinzani ni moja. Wao ni walalahai huku wananchi wakiwa walalahoi.

Kichungi kizuri cha kutenganisha punje halisi na makapi ni kutumia vigezo vya uadilifu na uaminifu wa wagombezi wa nyadhifa mbalimbali. Ni kwa kufanya hivi tu ndipo wananchi wataokoka dhidi ya utapeli wa wanasiasa.

Kipindi hiki cha uchaguzi watakuja kwa ahadi tele huku wakiwa wamejisahaulisha ahadi ambazo walizitoa kabla ya kuchaguliwa. Tuwakatae debeni. Tusihadaiwe na umaarufu wa vyama. Tuzingatie uadilifu na sera za wagombezi katika uchaguzi huu. Tusione shida kuwachagua watu faafu hata wakiwa wagombezi huru iwapo vyama vimejaa matapeli.

You can share this post!

Matiang’i ashutumu sheria kwa kuruhusu washukiwa kuwania

Muturi akataa stakabadhi zilizodai Ruto ni mnyakuzi

T L