• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
TAHARIRI: Uchaguzi: Raia waitikie wito wa kujitokeza kwa wingi wiki ijayo

TAHARIRI: Uchaguzi: Raia waitikie wito wa kujitokeza kwa wingi wiki ijayo

NA MHARIRI

ZIMESALIA siku za kuhesabika tu ili Wakenya wafanye uamuzi muhimu kwa kushiriki uchaguzi mkuu.

Siku ya siku yenyewe ni Jumanne ijayo, tarehe 9 Agosti, siku inayosubiriwa kwa hamu na ghamu wawaniaji nao wakishika roho mkononi kuhusu hatima yao katika ulingo wa siasa.

Wakenya nao watakuwa wakichagua viongozi wao kwa miaka mitano ijayo akiwemo rais wa tano baada ya kustaafu rais wa sasa Uhuru Kenyatta.

Ni shughuli isiyokuwa na utani kwa sababu itaamua mwelekeo ambao nchi itachukua kiuchumi, kijamii, kisiasa na mfumo mzima wa utawala.

Suala la uchaguzi mkuu si la kuchukuliwa kwa urahisi au kupuuzwa jinsi baadhi ya watu wanavyofanya.

Serikali ijayo iko mikononi mwa zaidi ya wapigakura milioni 22 ambao wamesajiliwa na Tume ya Uchaguzi (IEBC).

Hapa kuna mambo mawili; kukosa kujitokeza kupiga kura na kujitokeza kupiga kura. Kukosa kujitokeza kutaamanisha kuwa unakubali yeyote atakayechaguliwa na sera zake bila kujali athari zake kwa nchi na kwako binafsi.

Wanaofanya hivyo hawafai kulalamika viongozi wabaya wakiingia madarakani.

Hata hivyo, wao ndio huwa wanalalamika zaidi mambo yanapoenda kombo wakilaumu viongozi kwa sera zao.

Kama wangejitokeza, pengine kura yao moja, ingeleta mabadiliko makubwa kwa mwelekeo wa nchi.

Wanaojitokeza kupiga kura huwa na sababu ya kuwakosoa viongozi waliowachagua wakienda kinyume na viapo vya ofisi au wasipotimiza ahadi wanazowapa wakati wa uchaguzi mkuu.

Hii ni kwa sababu huwa wana ujasiri wa kutekeleza haki yao ya demokrasia. Haki hii haihitaji woga; woga ni adui wa demokrasia.

Msingi wa demokrasia ni wengi wape na wachache kubaki watazamaji hata kama ndio wenye haki.

Wengi wakichagua viongozi wabaya kwa sababu ya kujitokeza kwa wafuasi wa wale wazuri, nchi huwa inatumbukia kwenye shida huku kila mmoja akiumia.

Njia ya kuepuka hali hii ni kuwa na ujasiri wa kujitokeza kupiga kura kushiriki katika kuamua serikali ijayo.

Hili litatuepushia lawama za kila mara ambazo tunawalimbikizia hasa viongozi tuliochagua utendakazi wao unapokuwa hauridhishi kamwe.

  • Tags

You can share this post!

Ruto, Raila wapanga kulalamikia matokeo

Talanta ya soka ilimpa fursa ya kusoma kupitia ufadhili na...

T L