• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 5:23 PM
Ruto, Raila wapanga kulalamikia matokeo

Ruto, Raila wapanga kulalamikia matokeo

NA CHARLES WASONGA

MIRENGO ya Azimio na Kenya Kwanza (KKA) imeanza kujiandaa kwa mapambano katika Mahakama ya Juu, ishara kwamba kila mrengo hauko tayari kukubali matokeo ya uchaguzi mkuu wa Jumanne ijayo.

Kando na kuunda makundi ya mawakili wa kuwatetea katika mahakama hiyo, imeibuka kuwa kambi za Raila Odinga (Azimio) na William Ruto (KKA) zimeanza kukusanya ushahidi watakaotumia katika kesi zao za kupinga matokeo.

Wakati wa mdahalo wa urais Jumanne wiki iliyopita, uliosusiwa na Bw Odinga, Dkt Ruto alidokeza kuwa ataelekea katika Mahakama ya Juu kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais endapo atahisi kushindwa kwa njia isiyo halali.

“Ndio nitakubali kushindwa. Lakini nitawasilisha kesi mahakamani kupinga matokeo hayo endapo nitahisi kutotendewa haki. Kwenda kortini ni sawa na kukubali matokeo,” Dkt Ruto akasema.

Kwa upande wake, Bw Odinga amekuwa akishikilia kuwa atakubali matokeo ya uchaguzi wa urais kwa sharti kwamba uchaguzi huo utaendeshwa kwa njia huru na haki, ingawa haelezi vigezo atakavyotumia kuamua iwapo uchaguzi utamridhisha.

Kulingana na wadadisi, kauli hii ya Bw Odinga inaashiria kuwa ataelekea katika Mahakama ya Juu kupinga matokeo endapo atashindwa.

Pia kulingana na historia yake ya kuwania urais, Bw Odinga hajawahi kukubali kushindwa katika chaguzi nne ambazo ameshiriki mnamo 1997, 2007, 2013 na 2017.

Alipofaulu kuchangia kubatilishwa kwa matokeo ya urais 2017 alikataa kushiriki marudio ya uchaguzi huo.

Duru zimeambia Taifa Leo kwamba mawakili wanaoandaliwa na mirengo ya Azimio na Kenya Kwanza kuwawakilisha katika Mahakama ya Juu ndio wameteuliwa kuwa maajenti wakuu katika uchaguzi wa urais.

Kuteuliwa huko kumewaweka katika nafasi bora ya kufuatilia kwa makini mchakato mzima wa maandalizi, upigaji kura na ujumuishaji wa kura katika kituo cha kitaifa cha kujumuisha kura za urais katika Bomas of Kenya, Nairobi.

Katika mrengo wa Bw Odinga, jopo lake la mawakili linaongozwa na mshauri wa masuala ya sheria kwa kipindi kirefu Paul Mwangi.

Bw Mwangi anasaidiwa na Ajenti Mkuu wa mgombea urais huyo wa Azimio, Saitabao Kanchory, ambaye pia ni wakili.

“Raila ameteua mawakili kuwa maajenti wake katika ngazi ya kitaifa, katika kaunti zote 47 na katika maeneo bunge yote 290. Kibarua chao ni kukusanya data na ushahidi wowote ambao utatusaidia kujenga kesi yetu mahakamani,” akasema afisa mmoja wa ODM.

Katika kambi ya Dkt Ruto, maandalizi ya mapambano katika Mahakama ya Juu yamekuwa yakiendelea kwa muda mrefu, kulingana na mmoja wa wataalamu wa masuala ya sheria katika makao makuu ya UDA.

“Kila mtu anajiandaa. Chama chochote cha kisiasa kinachopania kutwaa uongozi sharti kijiandae kwa chochote ambacho kitatokea. Tunatarajia mpito mzuri, lakini ikiwa kutatokea haja, haitakuwa jambo la busara kukosa kujiandaa,” Dkt Musumba akanukuliwa akisema, bila kutoa ufafanuzi zaidi.

Hata hivyo, duru zilisema kuwa kundi la mawakili lililozinduliwa na Katiba Mkuu wa UDA, Veronica Maina mnamo Desemba 21, 2021 ndio wanatarajiwa kuongoza kesi ya Dkt Ruto katika Mahakama ya Juu.

Kundi hilo la mawakili 50 linaongozwa na wakili Georgiadis Majimbo na aliyekuwa Rais wa Chama cha Mawakili Nchini (LSK) Nelson Havi.

Wakili Mkuu Ahmednassir Abdullahi pia ni mwanachama wa jopo hilo.

“Tunajiandaa kutetea ushindi wetu na endapo tutapoteza, sharti tutambue hitilafu na kujenga ushahidi wetu kabla ya kupinga matokeo. Tuko na watu katika maeneo bunge yote 290 ambao wametwikwa wajibu wa kukusanya ushahidi,” akasema Bw Majimbo.

Kulingana na mchanguzi wa masuala ya sheria Bobby Mkangi, mirengo ya Dkt Ruto na Bw Odinga sharti ijiandae kwa kesi katika Mahakama ya Juu, kupinga matokeo au kutetea ushindi.

“Katiba inatoa nafasi kwa aliyeshindwa katika kinyang’anyiro cha urais kuwasilisha kesi katika Mahakama ya Juu endapo atahisi kutotendewa haki,” anasema Bw Mkangi, ambaye ni mmoja wataalamu walioandika Katiba ya sasa.

“Bila shaka mmoja kati ya Ruto na Raila ndiye ataibuka mshindi katika uchaguzi huu. Kwa hivyo, sharti wajiandae kisheria,” anaongeza Bw Mkangi.

Mwezi Julai, Jaji Mkuu Martha Koome alitangaza kuwa majaji wa Mahakama ya Juu wamepokea mafunzo maalum kwa matarajio kuwa kesi ya kupinga matokeo ya urais itawasilishwa mbele yao.

  • Tags

You can share this post!

Mama ashauri korti imnyime mwanawe dhamana kwa sababu ya...

TAHARIRI: Uchaguzi: Raia waitikie wito wa kujitokeza kwa...

T L