• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 3:31 PM
TAHARIRI: Wagombeaji urais wasifiche masuala mazito

TAHARIRI: Wagombeaji urais wasifiche masuala mazito

NA MHARIRI

MDAHALO mkali ambao unaendelea kushuhudiwa nchini kuhusu manifesto ya mwaniaji urais kwa chama cha kisiasa cha Muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya, ni suala linalotia moyo kuhusu ukomavu wa siasa za humu nchini.

Hii ni kutokana na ukweli kuwa, tangu muungano huo unaoongozwa na kinara wa ODM, Bw Raila Odinga, ulipotoa rasmi manifesto yake, wananchi wanazidi kuibua maswali kuihusu.

Yale tunayoona kwa sasa ni tofauti na hali iliyokuwepo ya manifesto kutolewa kwa shamrashamra tele kisha yaliyomo yakasahaulika mara moja hadi baada ya uchaguzi.

Hata hivyo, kinachosikitisha ni jinsi wananchi wengi na viongozi wa upande pinzani wanavyojikita sana kwenye suala moja pekee. Suala hilo linahusu mitumba.

Bila shaka ilitarajiwa kuwa suala hilo lingeibua hisia tele tofauti kwani hata Bw Odinga alipolitaja, alionekana kulazimika kueleza kwa undani zaidi alichomaanisha kuhusu pendekezo la marufuku ya mitumba nchini.

Ingalikuwa bora zaidi kama mijadala unaoendelea wa manifesto hiyo ingegusia masuala mengine mbali na mitumba kama vile mikakati ya uzalishaji chakula cha kutosheleza mahitaji ya wananchi, usambazaji maji safi nyumbani katika maeneo ambayo yanakumbwa na uhaba wa kila mara, uimarishaji wa usalama katika sehemu za nchi zinazokumbwa na mashambulio na mauaji ya mara kwa mara, uboreshaji wa huduma za afya ya umma, elimu miongoni mwa mengine.

Haya ni masuala mazito ambayo hayafai kupuuzwa wakati tunapojadiliana kuhusu mipango ambayo viongozi wa kisiasa wanaweka kuelekea kwa Uchaguzi Mkuu.

Inafaa mwananchi ajue kuhusu jinsi mambo haya yote yatakavyosuluhishwa kwani kumekuwa na ahadi tele tangu zamani zisizotimizwi. Mwananchi anaweza kuridhishwa au kukosa kuridhishwa na ahadi za kisiasa kulingana na midahalo itakayoibuka kuhusu ahadi hizo.

Mbali na hayo, mijadala hii inayoendelea imetuonyesha kuwa ni muhimu kwa wanasiasa hasa wagombeaji urais na ugavana kutoa manifesto zao mapema ili wananchi na wadau wengine wa uongozi wapate muda wa kutosha kutathmini mapendekezo yaliyomo.

Kwa njia hii, wananchi, wakiwemo wale ambao hudai kuwaachia viongozi wao wawasomee stakabadhi muhimu za kitaifa, watapata muda wa kudadisi manifesto hizo sio kwa kusoma au kusikia maelezo ya pande wanazoegemea pekee bali pia kuzingatia ukosoaji wa msimamo wao.

Mwelekeo huu utawawezesha wananchi wanaojali umuhimu wa kuwepo kwa viongozi bora mamlakani kuweka kwenye mizani maoni tofauti yanayotolewa na hatimaye kujiamulia kuhusu ukweli uliopo.

You can share this post!

Aliyeachiliwa na Rais asakwa kwa mauaji ya mamaye

WANDERI KAMAU: Wanasiasa wanaoghushi vyeti wanaharibu...

T L