• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 3:24 PM
WANDERI KAMAU: Wanasiasa wanaoghushi vyeti wanaharibu mwelekeo wa nchi

WANDERI KAMAU: Wanasiasa wanaoghushi vyeti wanaharibu mwelekeo wa nchi

NA WANDERI KAMAU

WAKENYA wengi wamelelewa wakifahamu kuwa njia ya pekee ya kufanikiwa maishani ni kupitia elimu.

Wengi walitia bidii masomoni mwao, ili kuhakikisha kuwa mbali na kutimiza ndoto zao maishani, wameboresha maisha ya wazazi na familia zao kwa jumla.

Wengi wana simulizi za kuatua moyo, kuhusu jinsi walivyojinyima raha na mambo mengi katika shule za msingi, upili na vyuo vikuu, ili kuepuka vikwazo vyovyote ambavyo vingewazuia kutimiza ndoto zao.

Kauli kuhusu umuhimu wa masomo ni jambo ambalo limepitishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Hata hivyo, inasikitisha kuwa licha ya maelfu ya vijana kuweka bidii kufanikiwa masomoni, baadhi ya wanasiasa wamefanikiwa kuchaguliwa na kuhudumu kwa mihula kadhaa bila kutimiza viwango vya kimasomo vinavyohitajika.

Kinaya ni kuwa, baadhi yao ni watu maarufu na waliojijengea majina makubwa katika ulingo wa siasa kwa muda mrefu sana.

Wakati habari kama hizi zinapoibuka katika nchi ambako mamilioni ya vijana hawana ajira licha ya kusoma, inawaatua moyo wengi wao.

Maelfu ya vijana nchini wamejihini mengi maishani, kwa kurudi vyuoni na kujiendeleza kimasomo kwa kufanya shahada za uzamili au uzamifu.

Licha ya juhudi hizo zote, wengi wao bado hawana ajira!

Katika nchi inayosisitiza umuhimu wa masomo kwa vizazi vyake vilivyopo na vinavyochipuka, huu ni mwelekeo hatari.

Ni mwelekeo unaoashiria kuwa tu nchi ambayo haijajitayarisha kushughulikia maslahi ya vizazi vyake vijavyo. Wakati vijana wanapowaona watu ambao hawakusoma wakifanikiwa maishani bila kupitia taratibu zinazofaa, wengi wao wamekuwa wakibuni “njia za mkato” kufaulu.

Baadhi yao wamekuwa wakitumia ujuzi walio nao kujiingiza kwenye vitendo vya uhalifu.

Si mara moja tumesikia vijana waliosoma wakikamatwa kwa kuingilia mitambo ya benki na kupora mamilioni ya pesa.

Ikizingatiwa wengi wana utaalamu mkubwa kwenye masuala ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia (ICT), si vigumu nchi kuendelea kushuhudia visa kama hivyo.

Kuna hatari vijana hao kugeuka kuwa “janga” kwa nchi na jamii kwa jumla, ikiwa uongozi uliopo hautabuni sera mwafaka zitakazohakikisha wamepata ajira kuendeleza ujuzi wao.

Ujumbe mkuu ambao vizazi vilivyopo vinapata vinapowaona wanasiasa waliofanikiwa maishani kwa kutofuata taratibu zifaazo ni kwamba, sisi tu jamii ambayo mtu anaweza kufanikiwa maishani kwa kutumia njia yoyote ile. Tu jamii ambapo bidii haitiliwi maanani hata kidogo. Tu jamii ambapo udanganyifu na ulaghai vimeibuka kuwa “nguzo” kuu za kufaulu maishani.

Katika taswira hiyo, je, jamii ina haki yoyote kuwalaumu vijana wanaotumia ujuzi walio nao kujitafutia riziki—hata ikiwa ni kwa njia za mkato?

Ingawa makala haya hayalengi kuushabikia wala kuuendeleza uhalifu kama njia ya kutafuta riziki, ujumbe wake mkuu ni kutoa onyo kwa jamii kutahadhari kuhusu hatari inayoikabili.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Wagombeaji urais wasifiche masuala mazito

BENSON MATHEKA: Inatia moyo kuona wanawake wakiwa katika...

T L