• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
TAHARIRI: Wahalifu wasitumie mahakama kama ngao

TAHARIRI: Wahalifu wasitumie mahakama kama ngao

NA MHARIRI

HATUA ya Mahakama ya Rufaa kuonya wanasiasa wanaokumbwa na mashtaka kutumia mbinu za kijanja kuidhinishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ni ya kutia moyo na inayopaswa kuungwa mkono na wote.

Katika siku za hivi karibuni, wanasiasa walioshtakiwa kwa makosa tofauti wamekuwa wakichelewesha kesi zao kimakusudi kwa lengo la kulemaza kesi hizo ndipo waweze kupata idhini ya IEBC kuwania nyadhifa mbalimbali uchaguzini.

Sheria iko wazi. Iwapo wewe ni mhalifu ambaye amepatikana na hatia mahakamani, basi huruhusiwi kuwania au kutetea kiti chako.

Kulingana na majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa, Wanjiru Karanja, Kathurima M’Inoti na Jamila Mohammed, baadhi ya wanasiasa ambao wamepatikana na hatia wamekuwa wakitumia mwanya kwenye sheria zetu ambapo mshtakiwa anaweza kuendelea na mchakato wa kusaka kura ilimradi amewasilisha rufaa katika mahakama ya juu kuliko iliyomhukumu.

Wengine wamekuwa wakichelewesha kesi zao, kwa ushirikiano na mawakili wao kwa kukwamisha kesi ili kipengee cha sheria kuhusu uadilifu kisiwafungie nje.

Isitoshe, wengine wao wamekuwa wakisingizia ugonjwa ili kuhakikisha kesi hizo hazipigi hatua zozote kortini. Matokeo yake ni kwamba, wahalifu ambao wanastahili kukaa jela wanapata fursa ya kuwania nyadhifa muhimu kama vile ubunge na hatimaye kutunga sheria ambazo hawaziheshimu.

Ni vipi raia wa kawaida wataheshimu na kuzingatia sheria za nchi wakati wanashuhudia viongozi waliohusishwa na kashfa kama uporaji wa mali ya umma, mauaji, unyakuzi ardhi na maovu mengine ya kijamiii wanatumia njia za mkato kuhujumu sheria?

Tunakubaliana kwa dhati na msimamo wa Mahakama ya Rufaa kwamba, ingawa Katiba inasema mshtakiwa aliyepatikana na hatia hawezi kuzuiwa kuwania wadhifa wa umma hadi fursa zote za kujitetea zikamilike, kuna vipengele vingine kwenye katiba ambavyo havipaswi kupuuzwa kutokana na mbinu za ulaghai ambazo baadhi ya wanasiasa waliofungwa na mahakama za chini wanatumia kuchelewesha kesi zao.

Ni matumaini yetu kwamba, mahakama zitasikiliza kesi na kutoa uamuzi kwa wakati ufaao ili wale wanaotekeleza uhalifu na kutumia mahakama kama ngao yao wakomeshwe.

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Dkt Ruto, wapi kiwanda cha kutengeneza...

Saba wakamatwa kwa madai ya wizi

T L