• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 10:55 AM
PETER NGARE: TSC ijue kuwa enzi za udikteta zilishakwisha

PETER NGARE: TSC ijue kuwa enzi za udikteta zilishakwisha

Na PETER NGARE

MIMI ni mwalimu aliyehitimu kufunza Kiswahili na Historia kutoka Chuo Kikuu cha Moi. Naam!

Lakini safari yangu ya kupata shahada ya Digrii ya Elimu, hasa nilipoenda kwa mazoezi ya kufunza katika shule ya Nambale Boys iliyoko Busia kisha Ossen Secondary katika Kaunti ya Baringo, ilinifanya niazimie kuwa nikifuzu sitatia guu langu darasani kufunza.

Sio eti singependa kufunza, bali niliona mazingira ya walimu kutiwa baridi ya kujieleza hayangenifaa.

Ndiposa nilipofuzu tu nilijitosa katika uanahabari, ambao nilihisi ungenipa uhuru wa kujieleza pamoja na kutetea maslahi ya mwananchi dhidi ya dhuluma za walio madarakani.

Matukio ya majuzi katika Tume ya Huduma za Walimu (TSC) hasa chini ya uongozi wa Bi Nancy Macharia yananifanya kuridhika kwamba sikufanya uamuzi mbaya.

Chini ya usimamizi wa Bi Macharia, TSC imewasukuma walimu kwenye kona kwa kuwazima midomo, na kuadhibu yeyote anayejaribu kukosoa maamuzi yake.

Kwanza ilikuwa ni kufifisha nguvu chama cha KNUT.

Kisha kumefuatia maamuzi ambayo walimu wanahitajika kuzingatia bila kusema ng’we!

Na la majuzi kabisa ni kuadhibu kwa kuwahamisha kiholela viongozi wa vuguvugu la Teachers Pressure Group (TPG).

Kulingana na TSC, kosa la maafisa wa TPG ni kuomba kutathminiwa upya kwa mpango wa matibabu chini ya kampuni ya Aon Minet, kutokana na kile wanasema ni huduma duni kwa walimu.

Kwa meneja yeyote anayejali wafanyakazi wake, busara ingekuwa ni kuwasikiza na kwa pamoja kupata suluhu bali sio kuwaadhibu.

Uongozi wa TSC unapasa kutambua kuwa enzi za giza la udikteta zilifika kikomo yapata miaka 30 iliyopita, na hivyo kujaribu kusimamia walimu kwa mabavu ni jambo ambalo halitafua dafu.

Demokrasia, uhuru na uwazi katika usimamizi wa taifa hautarajiwi tu katika uongozi wa kisiasa pekee, bali pia katika taasisi zingine za umma na hata za kibinafsi.

Meli ya kuheshimu haki za wafanyakazi kwa kuwatendea haki katika kila safu ya uajiri iling’oa nanga kitambo, na TSC kujaribu kuirudisha Kilindini sasa ni kibarua kigumu.

Ingawa kila meneja ana staili yake ya uongozi, sharti mtindo ambao meneja hasa wa kiwango cha CEO uzingatie heshima kwa wafanyakazi na kujali maslahi yao.

Ualimu sio utumwa bali ni taaluma ya kuheshimika na kuenziwa kutokana na mchango wake katika jamii. Sisi wote tupo tulipo kwa mchango wa walimu kuanzia chekechea hadi vyuoni.

Hivyo kuonyesha walimu madharau yasiyo kifani kwa kuwashinikizia bila hata kuwasikiza, na wanapofungua midomo unawaadhibu, ni jambo ambalo limepitwa na wakati.

Walimu pia ni kielelezo mashinani kwa jamii, na unapowajaza hofu na kuwadhalilisha unabomoa msingi huu muhimu katika mshikamano na ustawi wa kijamii.

TSC pamoja na Wizara ya Elimu sharti watambue kuwa hakuna mafanikio ya kujivunia watapata kwa kutumia mtindo wa kuwahofisha walimu.

Muda wa viongozi wa sasa wa TSC siku moja utafika kikomo, lakini wasipokomesha usimamizi wa kidikteta wataingia kwenye kumbukumbu za kihistoria kama waliovuruga taaluma ya ualimu na elimu kwa jumla hapa Kenya.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Wazazi, walezi wazungumze na watoto wao likizo...

Mkuu wa DCI ahukumiwa miezi minne jela

T L