• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
TAHARIRI: Wazazi, walezi wazungumze na watoto wao likizo hii fupi

TAHARIRI: Wazazi, walezi wazungumze na watoto wao likizo hii fupi

Na MHARIRI

KATIKA siku za hivi karibuni, wanafunzi wa shule mbalimbali nchini wamekuwa wakijihusisha na uchomaji wa shule na mabweni kila uchao na hili limewakosesha usingizi walimu, wazazi na jamii kwa jumla.

Shule zinafungwa leo kwa likizo fupi na yatarajiwa kuwa wanafunzi watakaa na wazazi na walezi wao na kubadilishana mawazo yanayohusu maisha yao shuleni.

Waketi na wana wao na kuwadadisi kuhusu matatizo yanayowakumba na kuwapa ushauri nasaha pamoja na kuwakidhia mahitaji yao ili kuepusha ghasia na visa vya kuteketeza mali ya shule.

Lakini kabla ya kulaumu wanafunzi wanaotekeleza uovu huu, jamii yetu inafaa kuzinduka mapema na kujiuliza maswali yafuatayo; Je, kwa nini wanafunzi ambao ni watoto wetu wawe wajasiri kuteketeza mabweni?

Je, kwa nini wanafunzi ambao umri wao ni mdogo wanahusika katika uhuni na uhalifu huu bila kuogopa?

Je, wanafunzi hawa watundu wanajua uchungu wa jamii katika kugharimia ukarabati wa madarasa ambayo walichoma? Haya ni maswali ambayo yanafaa kujibiwa na jamii bila kusutana au kutupiana lawama.

Tuchukue hatua kuokoa hali isiyumbe zaidi. Hata hivyo, tangazo la waziri wa Elimu Profesa George Magoha kuwatwika mzigo mzito wazazi kugharimia ukarabati na ujenzi wa majengo yanayoteketezwa na wanafunzi lasikitisha na kuatua moyo.

Si hatua ya busara na tangazo hilo halitaisaidia lolote bali litazidisha malumbano baina ya serikali, wazazi na hata walimu.

Mzazi hapaswi kubebeshwa zigo la dhambi za mwanawe shuleni.

Tunahitaji kuwa na njia mbadala ya kushughulikia zahama hii.

Kuwajibisha wazazi kutokana na utundu wa wanao hakutakomesha visa hivyo vya kihuni katika shule husika.

Serikali haifai kutumia visa vya wanafunzi wakora kuwaumiza wazazi ambao wamelemewa na maisha kiuchumi kiasi cha kuishi kuhangaika na kujinyima ili kugharimia elimu ya watoto wao ambao baadhi yao wamegeuka wahuni wanyama wanaosababisha uharibifu shuleni bila kujali madhara.

Ikiwa wazazi watalazimishwa kulipia ujenzi wa mabweni mapya, watakosa nafasi nzuri ya kushirikiana na walimu na washikadau wengine wa elimu mashinani na kitaifa kusaka suluhisho la kudumu kukabili janga hili ibuka.

Tangazo la waziri Magoha lilipaswa kuimarisha juhudi za kukomesha ukaidi huu wa wanafunzi kuchoma shule, kuzua rabsha, kugoma na kuharibu mali shuleni kama njia ya kuelezea udhia wao au matatizo yanayowasumbua bila kutatuliwa na wakuu wa shule.

Siku hizi chache zitumiwe na wazazi na watoto wao kujadili njia mwafaka za kusuluhisha shida zao badala ya kuvamia mali ya shule. na kuiharibu pasi na kujutia makosa hayo.

You can share this post!

kinoti kufungwa miezi minne gerezani

PETER NGARE: TSC ijue kuwa enzi za udikteta zilishakwisha

T L