• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
WASONGA: Wanasiasa wakome siasa za kuwachochea Wakenya

WASONGA: Wanasiasa wakome siasa za kuwachochea Wakenya

Na CHARLES WASONGA

KUNA kila dalili kwamba mirengo mikuu ya kisiasa nchini inawachochea wananchi kuzua fujo baada ya matokeo ya urais kutangazwa.

Kila mrengo unaonekana kuandaa wafuasi wao kutokubali matokeo endapo mgombeaji wao hatatangazwa mshindi katika kinyang’anyiro hicho mwaka 2022.

Kwanza, mnamo Ijumaa Rais Uhuru Kenyatta aliwaonya Wakenya dhidi ya wezi ambao watapora mali ya taifa hili na kurudisha nyuma rekodi yake ya maendeleo na ile ya mtangulizi wake, Rais mstaafu Mwai Kibaki.

Bila shaka kiongozi wa taifa alitoa kauli hiyo katika muktadha wa siasa za urithi wa kiti chake ambazo zimeshika kasi wakati huu.

Kwa hivyo, Rais Kenyatta, ambaye alitoa kauli hiyo akiwa Ruiru, Kiambu, alikuwa akiwaonya wananchi kutowachagua wagombeaji fulani wa urais, ambao kwa mtazamo wake, ni wezi. Hakutoa ithibati.

Kwa mtazamo wangu, huu ni uchochezi kwa sababu ni haki ya Wakenya, kwa mujibu wa kipengele cha 38 cha Katiba, kumchagua mgombeaji yoyote wa urais wanayemtaka.

Muhimu ni kwamba mwanasiasa huyo aidhinishwe na asasi zote husika za serikali pamoja na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwa mujibu wa Katiba na sheria husika.

Pili, mrengo wa Naibu Rais William Ruto umeanzisha kampeni chafu ya kumsawiri kiongozi wa ODM Raila Odinga kama “mradi wa serikali” katika siasa za urithi wa urais.

Kimsingi, Dkt Ruto na wandani wake wanadai Bw Odinga anapendelewa na Rais Kenyatta na watu wenye ushawishi mkubwa serikalini, almaarufu, “Deep State”.

Kwa mtazamo wangu, hii ina maana kuwa endapo Waziri huyu mkuu wa zamani ataibuka mshindi katika uchaguzi wa urais mwaka 2022, Dkt Ruto na wafuasi wake watakuwa na kila sababu ya kudai kuwa ushindi huo ni haramu.

Kwamba nguvu za dola zilitumika kushawishi matokeo kama hayo.

Hali kama hii inaweza kusababisha fujo nchini sawa na ilivyokuwa baada ya uchaguzi mkuu wa 2007.

Isitoshe, kama ishara ya kuhimili dhana kwamba Bw Odinga ni “mradi wa serikali”, wabunge Ndindi Nyoro (Kiharu), Nderitu Gachagua (Mathira), Alice Wahome (Kandara) na Seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata, wamedai kampeni zake zinapigwa jeki na mawaziri, Dkt Fred Matiang’i na Bw Joe Mucheru.

Wanasiasa hawa wanawataka mawaziri hawa wajiuzulu kwa kugeuka kuwa “maajenti wa ODM” ilhali wizara zao zinahusika moja kwa moja na maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Madai ya wandani hawa wa Dkt Ruto yana mashiko kwa sababu Dkt Matiang’i anaongoza Wizara ya Usalama inayosimamia vikosi vyote vya polisi wenye wajibu wa kudhibiti usalama wakati wa uchaguzi mkuu.

Naye Bw Mucheru anaongoza Wizara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) inayosimamia Tume ya Mawasiliano Nchini (CA) ambayo IEBC itategemea kufanikisha upeperushaji wa matokeo ya uchaguzi.

Lakini ikiwa Dkt Ruto na chama cha United Democratic Alliance (UDA) ni maarufu miongoni mwa wapiga kura jinsi wakereketwa wa vuguvugu la “The Hustler Nation” wanadai, basi hawafai kuingiwa na baridi.

Naibu Rais atashinda urais hata kama Mbw Matiang’i na Mucheru wataendelea kushikilia nyadhifa zao.Wakumbuke kuwa Mzee Kibaki alishinda urais mnamo 2002 chini ya mwavuli wa muungano wa NARC licha ya kwamba Rais Kenyatta wakati huo alikuwa “mradi wa serikali” na chaguo la marehemu Daniel Moi aliyedhibiti asasi zote za serikali, hususan zile za usalama.

Mrengo wa One Kenya Alliance (OKA) nao ukome kudai kuwa vinara wake wanapigiwa simu kushurutishwa wamuunge mkono mgombea urais fulani.

Aidha, vinara wa muungano huo wakome kudai kuwa kuna njama ya kuwalazimishia Wakenya mtu fulani awe Rais wao.

Kwa mtazamo wangu, huu ni uchochezi.

  • Tags

You can share this post!

Jinsi ya kuandaa milkshake ya tende

Uchaguzi mdogo Ukambani wampa Ruto ujasiri

T L