• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
WANDERI KAMAU: Kenya sasa ilenge kuboresha mitambo kuondoa hofu ya udukuzi uchaguzini

WANDERI KAMAU: Kenya sasa ilenge kuboresha mitambo kuondoa hofu ya udukuzi uchaguzini

NA WANDERI KAMAU

KILA uchaguzi mkuu unapofanyika nchini, hakukosi kuwa na madai ya udukuzi wa mitambo ya watu wanaosimamia uchaguzi huo.

Mnamo 2017, kuliibuka madai ya udukuzi yanayodaiwa kuendeshwa na kampuni ya Cambridge Analytica kutoka nchini Uingereza.

Baadhi ya ripoti zilidai kuwa kampuni hiyo ndiyo iliyokisaidia chama cha Jubilee chake Rais Mstaafu Uhuru na Rais William Ruto (wakati huo akiwa Naibu Rais) kuibuka mshindi kwenye uchaguzi huo.

Inaelezwa kuwa hiyo ndiyo moja ya sababu zilizoifanya Mahakama ya Upeo, hasa Jaji Mkuu Mstaafu David Maraga kufutilia mbali uchaguzi huo, kufuatia kesi iliyowasilishwa na mrengo wa Nasa, wakati huo ukiongozwa na Raila Odinga.

Kama hilo halitoshi, madai hayo yameibuka tena.

Mara hii, inadaiwa kuwa wadukuzi kutoka nchini Israeli walifanikiwa kudukua mitambo ya baadhi ya maafisa wakuu wa mirengo ya Azimio la Umoja na Kenya Kwanza.

Katika kile kinachoonyesha madai hayo kuwa ya kweli, baadhi ya mabloga wanaoegemea mrengo wa Kenya Kwanza wamekiri kuwa mitambo yao iliingiliwa katika hali tatanishi na watu wasiowajua.

Katika hali hii, ni wazi kusema kuwa kiwango cha usalama wa mitambo yetu ya kiteknolojia ni cha kutiliwa shaka ikiwa raia wa kigeni wana uwezo kuiingilia na kuivuruga bila ufahamu wa watu husika.

Bila shaka, hii ni changamoto kuu kwa serikali na wadau wote husika kuwekeza katika kuimarisha usalama wa mitambo hiyo ili kuepuka marudio ya tukio kama hilo.

  • Tags

You can share this post!

Shule 90 zafungwa baada ya mafuriko kuathiri miji

NYOTA WA WIKI: Alejandro Garnacho

T L