• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 1:01 PM
Shule 90 zafungwa baada ya mafuriko kuathiri miji

Shule 90 zafungwa baada ya mafuriko kuathiri miji

NA MASHIRIKA

MAPUTO, MSUMBIJI

SERIKALI ya Msumbiji imesitisha masomo kwa shule 90 za msingi na upili katika maeneo yaliyoathirika na mafuriko.

Katika taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari, masomo hayo yalisitishwa kwa muda wa siku saba.

“Shule zilizoko katika miji ya Boane, Namaacha, Magude na Manhica zitasitisha masomo kwa siku saba kuanzia leo (Alhamisi),” akasema Gavana wa mkoa wa Maputo Julio Parruque katika taarifa hiyo.

Alisema hayo baada ya kuongoza mkutano na wadau katika sekta ya elimu kufuatia mvua kubwa, inayoandamana na upepo, inayoshuhudiwa nchini humo.

Data kutoka kutoka Taasisi ya Kitaifa ya Kupambana na Majanga (INGD), zinaonyesha kuwa watu tisa walikufa na wengine 39,225 wakaathirika na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyoanza kushuhudiwa Msumbiji Februari 7.

Msumbiji ni mojawapo ya nchi maskini zaidi ulimwenguni huku watu wengi wakiishi kwa chini ya dola moja kwa siku.
Imeorodheshwa nambari 181 miongoni mwa mataifa 189 maskini, kulingana na orodha ya kitengo cha maendeleo ya kibinadamu katika Umoja wa Mataifa (UN).

Kwingineko, Umoja wa Mataifa unaomba msaada wa dola 1.3 bilioni za Amerika (Sh162.5 bilioni) kufadhili shughuli za kutoa msaada kwa raia milioni sita nchini Nigeria, wanaoteseka kutokana na makali ya mashambulio ya wanamgambo wa kiislamu kaskazini mwa nchi hiyo.

Mashirika ya kutoa misaada yanasema, wapiganaji wa kundi la Boko Haram, na tawi lake, Islamic State West Africa Province (ISWAP) , wamekuwa wakipigana na wanajeshi wa Nigeria kaskazini mwa nchi hiyo kwa miaka 10 ambapo wameua mamia ya raia huku zaidi ya watu milioni mbili wakitoroka makwao.

Matthias Schmale, mshirikishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) la kutoa misaada Nigeria, alisema changamoto zinazowakumba waathiriwa wa machafuko hayo “hazijaonyesha dalili za kupungua”.

UN inasema idadi ya watoto wanaoteseka kutokana na utapiaji mlo inakadiriwa kuongezeka hadi kufikia milioni mbili mwaka huu, kutoka 1.74 milioni mwaka 2022.

“Wanawake na wasichana wadogo ndio wameathirika zaidi,” Schmale akasema alipokuwa akizindua msaada wa kifedha katika jimbo la Adamawa, lililoko Kaskazini-Mashariki mwa Nigeria.

Alisema asilimia 80 ya watu, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wanahitaji misaada katika majimbo ya Borno, Adamawa na Yobe.

“Wanaathirika na vita, utekaji nyara, ubakaji na dhuluma nyinginezo,” Schmale akaeleza.

Serikali ya Nigeria inasema inaelekea kushinda vita dhidi ya wanamgambo hao huku ikiongeza kuwa wanamgambo hao wametokomezwa kabisa kutoka maeneo waliyoteka. Inasema kuwa maeneo yaliyokombolewa sasa ni salama kwa wanakijiji kurejea ili waendelee na maisha yao ya kawaida.

  • Tags

You can share this post!

Wanawake washtuka kugundua waume wao ni mashoga

WANDERI KAMAU: Kenya sasa ilenge kuboresha mitambo kuondoa...

T L