• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
WANDERI KAMAU: Lilikuwa kosa kuwaogofya wanafunzi wa Gredi ya 6

WANDERI KAMAU: Lilikuwa kosa kuwaogofya wanafunzi wa Gredi ya 6

NA WANDERI KAMAU

UBORA ama ubaya wa kitu ama jambo lolote lile hubainika baada ya kufanyiwa majaribio kadhaa.

Bila majaribio hayo, ni vigumu sana kuamua ufaafu wake kwa jamii ama walengwa.

Katika sayansi, utafiti huwa kama kurunzi kuu inayotoa mwanga na mwongozo kuhusu matumizi ya dawa fulani miongoni mwa wanadamu ama wanyama.

Ikiwa matokeo ya utafiti yatabaini dawa husika haifai, basi huwa inaachwa na utafiti mwingine kuanza. Huo pia ndio mkondo wa kimaisha tunaopaswa kuzingatia na kufuata kama jamii.

Wiki iliyopita, watahiniwa milioni 1.2 walifanya Mtihani wa Gredi ya Sita (KPSEA) kote nchini, chini ya mazingira yenye utata kuhusu ikiwa wangejiunga na shule za upili au la, baada ya kuumaliza mtihani huo.

Ni utata ulioonekana kuwapa tumbojoto maelfu ya wazazi, baadhi wakisema umri wa watoto wao ni mdogo sana kuruhusiwa kujiunga na shule za sekondari.

Hata hivyo, Alhamisi iliyopita, Rais William Ruto aliondoa utata huo, aliposema kuwa watahiniwa hao watajiunga na Shule za Upili Tangulizi, zitakazokuwa katika shule zao za msingi. Hili linamaanisha wanafunzi hao wataendelea na masomo yao katika mazingira waliyokuwa wameyazoea.

Pia, Rais alitangaza kuwa Sekondari hizo Tangulizi zitajumuisha Gredi za Saba, Nane na Tisa, hilo likimaanisha kuwa wanafunzi watakuwa wakisoma katika shule za msingi kwa miaka tisa, kinyume na sasa ambapo huwa wanasoma kwa miaka minane.

Tangazo lake lilifuatia ripoti ya mpito iliyowasilishwa kwake na Jopo la Kushughulikia Mageuzi ya Elimu (PWPER), linaloongozwa na Prof Raphael Munavu.

Bila shaka, huku tangazo hilo likiwa afueni kubwa kwa wazazi na watahiniwa, kuna kosa kubwa lililotokea kwenye mchakato wa maandalizi, usimamizi na uendeshaji wa mtihani huo, ambalo halipaswi kurudiwa tena.

Kosa hilo ni kubuni mazingira ya kuwaogofya wanafunzi, kwa kuwatuma polisi waliojihami kuwalinda.

Kosa jingine ni kuufananisha mtihani huo na mitihani mingine ya kitaifa—yaani Mtihani wa Darasa la Nane (KCPE) au Kidato cha Nne (KCSE).

Kulingana na pendekezo la jopo hilo, KPSEA haitakuwa ikitumika kuwaorodhesha wanafunzi kulingana na matokeo yao, bali kutathmini maendeleo yao kimasomo na kutumia matokeo hayo kuwasaidia katika masomo watakayopatikana wakiwa na udhaifu.

Swali linaloibuka ni je, iwapo mtihani huu hautakuwa na umuhimu wa kitaifa, kuna haja ipi kuwatuma polisi, maafisa wa ngazi za juu serikalini (akiwemo rais) na wadau wengine kuusimamia?

Ni umuhimu upi uko katika kutumia mamilioni ya pesa kugharimia masuala ya usalama, usafirishaji na marupurupu ya wasimamizi wake ikiwa hautakuwa na umuhimu wa kitaifa?

Ukweli ni kuwa, huu ni mtihani unaoweza kuandaliwa na shule husika wanakosomea wanafunzi hao, kubaini maendeleo yao na kupata usaidizi binafsi kutoka kwa walimu wao.

Huu ulikuwa utumizi mbaya wa fedha za umma. Mitihani inayopaswa kusimamiwa kwa kiwango hicho ni KCPE ama KCPE kwani ni ya kitaifa na ina umuhimu mkubwa katika maisha ya baadaye ya wanafunzi husika.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Bajeti za kaunti zizingatie pia maoni ya umma

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Giroud avunja rekodi ya Thierry...

T L