• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 5:04 PM
WANDERI KAMAU: Mshindi wa urais ajihadhari na washirika wake wasimhujumu

WANDERI KAMAU: Mshindi wa urais ajihadhari na washirika wake wasimhujumu

NA WANDERI KAMAU

MNAMO 1917, Vladimir Lenin aliongoza maasi makali ya kisiasa dhidi ya utawala wa kifalme nchini Urusi, maarufu kama ‘Bolshevik Revolution.’

Lenin alikuwa miongoni mwa viongozi waliokuwa maarufu kwa raia waliohisi kuchoshwa na udhalimu wa mfumo wa kiutawala wa kifalme.

Ili kutimiza matakwa ya raia, miongoni mwa mageuzi ya kiutawala aliyoleta ni mfumo wa kisoshalisti, ambapo raia walipata nafasi ya kumiliki mali bila vikwazo vingi kutoka kwa serikali.

Ingawa mfumo huo ulisambaratika baadaye katika miaka ya tisini, ulilaumiwa kutekwa na baadhi ya viongozi ili kujitajirisha.
Nchini Tanzania, aliyekuwa kiongozi wa taifa hilo, Mwalimu Julius Nyerere, alijipatia umaarufu mkubwa miongoni mwa Watanzania, baada ya kuanzisha mfumo wa ujamaa miaka ya sitini, mara tu baada ya taifa hilo kupata uhuru wake kutoka kwa Uingereza. Awali, Tanzania ilikuwa ikitawaliwa na Wajerumani.

Hata hivyo, baada ya mfumo huo kutofaulu, Nyerere aliwaomba radhi Watanzania, akikiri kuwa mfumo haukuwiana na mwelekeo wa mataifa mengine duniani.

Mifano hiyo miwili inaashiria jinsi viongozi wanaopata umaarufu katika jamii zao kwa kubuni sera za kuwakomboa raia baadaye huangushwa na utekelezaji mbaya au washirika wao wa karibu.

Nchini Kenya, uchaguzi mkuu wa 2002 ni kati ya chaguzi zilizoashiria matumaini na mapambazuko makubwa ya kisiasa tangu tujinyakulie uhuru 1963.

Wakenya walipiga kura kwa ghadhabu kuuangusha utawala wa Kanu, baada ya kuiongoza nchi kwa karibu miaka 40, bila uwepo wa sera nzuri za kuwainua kiuchumi.

Ingawa utawala wa marehemu Mwai Kibaki ulitoa ahadi nyingi kwa Wakenya, nyingi hazikutimia baada ya “kutekwa” na baadhi ya washirika wake kupitia ufisadi.

Vivyo hivyo, lazima kiongozi atakayechukua usukani baada ya Rais Uhuru Kenyatta kung’atuka uongozini kufahamu kuwa, mipango na ajenda zake za maendeleo zinaweza kuvurugwa na washirika wake wenyewe.

Kwa mfano, Rais Mteule William Ruto ameahidi kuwainua kiuchumi Wakenya wa kiwango cha chini, kubuni Hazina Maalum ya Hustler, itakayotoa mikopo kwa raia kwa kiwango cha chini cha riba.

Vivyo hivyo, mwaniaji urais wa muungano wa Azimio-One Kenya, Bw Raila Odinga, ameahidi kutoa Sh6,000 kila mwezi kuzisaidia familia maskini ambazo hazijiwezi kiuchumi.

Bila shaka, hiyo ni mipango mizuri ya kiuchumi, ila lazima wahakikishe wameweka mikakati ifaayo kuhakikisha kuwa utekelezaji wake umefaulu.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

WANTO WARUI: Wanafunzi wa sekondari za chini wasichanganywe...

Mafuriko yaua watu zaidi nchini Pakistan

T L