• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:01 AM
Mafuriko yaua watu zaidi nchini Pakistan

Mafuriko yaua watu zaidi nchini Pakistan

NA MASHIRIKA

ISLAMABAD, PAKISTAN

PAKISTAN imeomba msaada zaidi kutoka kwa jamii ya kimataifa kukabili mafuriko yanayoendelea nchini humo, huku watu 119 zaidi wakithibitishwa kufariki.

Kulingana na Idara ya Kukabili na Kusimamia Mikasa nchini humo (NDMA), idadi ya watu waliokuwa wamefariki kufikia jana ilikuwa 1,033.

Kutokana na hali hiyo, watu walio katika maeneo yaliyoathiriwa wamelazimika kutafuta makao mbadala kwenye maeneo ya miinuko.

Amerika, Uingereza na Miliki ya Kiarabu (UAE) ni baadhi nchi ambazo zimetoa misaada yake, ijapokuwa maafisa wa serikali wanasema kuwa misaada zaidi bado inahitajika.

“Serikali ya Pakistan inafanya kila iwezalo kuwasaidia waathiriwa, ijapokuwa tunahitaji misaada zaidi kutoka kwa jamii ya kimataifa,” akasema Salman Sufi, kutoka kwa Wizara ya Usalama wa Ndani.

“Kama nchi, tumekuwa tukikabiliwa na changamoto za kiuchumi. Hata hivyo, inasikitika tumekumbwa na mkasa huu wakati hali hiyo ilikuwa ikiimarika,” akeleza.

Aliongeza kuwa fedha nyingi ambazo zilipangiwa kutumika kwenye miradi ya maendeleo zimeelekezwa katika shughuli za kuwasaidia waathiriwa wa mafuriko hayo.

Miongoni mwa maeneo yaliyoathiriwa ni mkoa wa Karachi.

Katika eneo la kaskazini mashariki mwa taifa hilo, maelfu ya watu walitoroka makwao baada ya mito iliyo katika mkoa wa Khyber Pakhtunkhwa kuvunja kingo zake na kusomba makazi.

“Nyumba tuliyojenga kwa kujitolea kwingi imeanguka mbele yetu tukiitazama,” akasema Junaid Khan, 23, kwenye mahojiano na wanahabari.

Mkoa wa Sindh, kusini mwa taifa hilo, pia ni miongoni mwa maeneo yaliyoathiriwa. Kama maeneo mengine, maelfu ya watu wameachwa bila makao.

Waathiriwa wa mafuriko walilazimika kupanga foleni ndefu ili kupokea usaidizi wa kifedha.

“Kulikuwa na watu walioachwa makwao katika sehemu zote tulizozuru katika mkoa wa Sindh. Bado haijabainika kiwango cha uharibifu kilichosababishwa na mafuriko hayo katika mkoa huo. Wenyeji wanayataja kuwa mabaya zaidi kuwahi kutokea,” akaeleza mwanahabari mmoja.

Ni nadra sana mafuriko kutokea nchini Pakistan, ijapokuwa waathiriwa wanataja mvua hiyo “kuwa tofauti.”

Mkazi mmoja alitaja mafuriko hayo kama “yale yaliyoelezwa kwenye Biblia.”

Karibu na jiji la Larkana, mamia ya nyumba za matope zimesomba na maji.

Mahitaji ya waathiriwa pia ni tofauti. Katika baadhi ya vijiji, wenyeji wanahitaji chakula kwa dharura. Katika vijiji vingine, wanasema wanahitaji msaada wa kifedha kukidhi mahitaji ya msingi, kwani tayari wana vyakula vya kutosha kwenye maghala yao.

Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, amesema kuwa jumla ya watu 33 milioni wameathiriwa na mafuriko hayo. Idadi hiyo inawakilisha asilimia 15 ya raia katika taifa hilo.

Alisema kuwa hasara iliyosababishwa na maafa hayo inalingana na yale yaliyotokea kati ya mwaka 2010 na 2011.

  • Tags

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Mshindi wa urais ajihadhari na washirika...

TALANTA: 4K Club ya aina yake

T L