• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
WANDERI KAMAU: Wanahabari waangazie wagombeaji kwa usawa

WANDERI KAMAU: Wanahabari waangazie wagombeaji kwa usawa

NA WANDERI KAMAU

VYOMBO vya habari ni miongoni mwa taasisi zitakazotekeleza majukumu muhimu kampeni za uchaguzi mkuu wa Agosti zinapoendelea kushika kasi.

Macho yote ya wananchi yataelekezwa kwa vyombo hivyo—hasa kuhusu vitakavyoangazia mirengo tofauti ya kisiasa ambayo ishaanza kampeni zao.

Katika nchi za Magharibi kama Amerika, vyombo vya habari ni miongoni mwa taasisi ambazo huchangia maamuzi ambayo raia hufanya, hasa kwenye uchaguzi wa urais.

Ili kuonyesha uzito wa majukumu ambayo huwa vinatekeleza, ni kawaida kwa vyombo hivyo kuchukua misimamo fulani ya kisiasa, ambapo hutoa sababu ni kwa nini kiongozi fulani anafaa kuchaguliwa kama rais na wala si mwingine.

Kwa mfano, kwenye uchaguzi wa urais nchini humo Novemba 2020, karibu mashirika yote makubwa ya habari yalimpinga vikali Donald Trump kuchaguliwa kwa muhula wa pili kama rais.

Mashirika hayo yalimlaumu Trump kwa kuonyesha ukatili dhidi ya wanahabari, kupuuzilia mbali athari za janga la virusi vya corona, kutoshughulikia ifaavyo visa vya weusi kubaguliwa na kuhangaishwa kwa misingi ya rangi yao, kati ya maovu mengine.

Mashirika makubwa ya uanahabari kama CNN, Fox News, CBS kati ya mengine yaliungana kumkosoa Trump kutokana na alikokuwa akielekeza Amerika.

Inaelezwa kando na raia wengi kutoridhishwa na uongozi wa Trump, misimamo ya mashirika hayo ilichangia sana maamuzi yao kutomuunga mkono kiongozi huyo.

Ingawa vyombo vya habari huwa havijitokezi wazi nchini kuonyesha misimamo yao ya kisiasa, baadhi vimelaumiwa kwa kuonyesha mapendeleo ya wazi dhidi ya mirengo fulani ya kisiasa.

Ingawa wakosoaji hao bado hawajajitokeza waziwazi kuthibitisha madai yao, si picha nzuri wakati raia wenyewe wanaanza kusikika wakitoa malalamishi ya kichinichini kutilia shaka uhuru wa baadhi ya mashirika ya habari.

Kwa miaka mingi, tafiti nyingi nchini zimekuwa zikiorodhesha vyombo hivyo kuwa miongoni mwa taasisi zinazoaminika zaidi na wananchi.

Katika maeneo ya mashambani, ambako mpenyo wa intaneti bado uko chini, wananchi hutegemea vyombo vya habari kama vile redio kufuatilia matukio yanayoendelea nchini na duniani kote kwa jumla.

Wengi wanaamini vyombo hivyo kama taasisi zinazoeleza ukweli kwa ukamilifu mkubwa.

Hivyo, ni makosa wakati vinaonekana kuvunja imani kama hiyo kwa kuanza kuonyesha misimamo fulani ya kisiasa, japo kwa njia fiche.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

81 wanyongwa nchini Saudia

Urusi yavamia eneo la kufunzia jeshi Ukraine

T L