• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Urusi yavamia eneo la kufunzia jeshi Ukraine

Urusi yavamia eneo la kufunzia jeshi Ukraine

NA MASHIRIKA

KYIV, UKRAINE

MAJESHI ya Urusi jana Jumapili yalianzisha mashambulio makali ya angani dhidi ya eneo moja la kutoa mafunzo kwa wanajeshi nchini Ukraine, lililo karibu na mji wa Lviv, ulio karibu na mpaka wa Poland.

Taarifa za serikali zilisema Urusi pia iliharibu uwanja mmoja wa ndege ulio katika mji wa Vasylkiv, kusini mwa taifa hilo.

Jumapili, mshauri wa Rais Volodymr Zelensky, Mykhailo Podolyak, alisema kuwa majeshi ya Urusi sasa yamefanikiwa kulizingira jiji kuu, Kyiv.

Hata hivyo, alisema raia wengi wamejitolea kuanza kuutetea mji huo kwa kila wawezalo dhidi ya kutekwa na wanajeshi hao.

Hayo yalijiri huku viongozi wa Ufaransa na Ujerumani wakimrai Rais Vladimir Putin wa Urusi kuyaondoa majeshi yake mjini Mariupol.

Majeshi hayo yamekuwa yakiuzingira mji huo kwa siku 11 mfululizo, ripoti zikiibuka kuwa wengi wanafariki kutokana na ukosefu wa maji na chakula.Meya wa mji huo alisema kuwa zaidi ya raia 1,500 wameuawa.

Miili mingi imeripotiwa kutapakaa barabarani bila kuchukuliwa na yeyote.Maafisa wakuu wa Ukraine na Urusi wametaja hali hiyo kuwa “ya kuhofisha.”

Ukraine inadai kuwa jeshi la Urusi lilirusha kombora kwenye msikiti ambako raia 80 walikuwa wametafuta hifadhi.

Hata hivyo, mkazi mmoja aliyekuwa karibu na msikiti huo alikanusha madai hayo, akisema kuwa kombora hilo lilianguka umbali wa mita 700 kutoka kwa msikiti huo.

Rais wa Amerika Joe Biden ameagiza Ukraine kupewa msaada zaidi wa kijeshi wa kiasi cha Sh20 bilioni.

Msaada huo ni nyongeza ya msaada mwingine wa Sh35 bilioni wa vifaa vya kijeshi ambao tayari Amerika imetoa.

Msaada huo unatajwa kuwa mkubwa zaidi kuwahi kutolewa na Amerika kwa nchi yoyote.

Idara ya Ujasusi ya Ukraine ilisema kuwa majeshi ya Urusi yalifyatulia risasi kundi moja la wanawake, ambapo ziliwaua saba kati yao, akiwemo mtoto mmoja.

Jumamosi, Naibu Waziri Mkuu wa Ukraine alisema kuwa jumla ya watu 13,000 wamefanikiwa kutorokea maeneo salama kwa kutumia vijia tisa kati ya 14 vilivyotengenezwa kuwawezesha wakimbizi walioathiriwa na mapigano kutorokea.

Kwa mara ya kwanza, Rais Zelensky alisema jumla ya wanajeshi 1,300 wa Ukraine wameuawa tangu mapigano hayo kuanza.

Wiki iliyopita, Urusi ilisema imewapoteza wanajeshi 498.

Hata hivyo, Zelensky amekuwa akisisitiza kuwa karibu wanajeshi 12,000 wa Urusi wameuawa.

Kulingana na Umoja wa Mataifa (UN), raia 579 wa Ukraine wameuawa.

Waziri Mkuu wa Ukraine, Denys Shmyhal, alisema kuna haja taifa hilo kuanza kujenga tena uchumi wake, kutokana na athari za vita hivyo.

Aliwarai watu walio katika maeneo ambamo hamna vita kurejelea kazi zao.

Majeshi ya Urusi pia yanalaumiwa kwa kushambulia kliniki moja ya macho katika mji wa Mykolaiv, siku chache baada ya kushambulia hospitali ya kujifungulia akina mama katika mji wa Mariupol.

Wakati huo huo, wabunge wa Ukraine walisema kuwa wanajeshi wa Urusi wamemteka meya wa mji wa Melitopol, Ivan Fedorov.

Wabunge hao walisema haikubainika mara moja alikopelekwa meya huyo.

  • Tags

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Wanahabari waangazie wagombeaji kwa usawa

Chepng’etich arejea Japan kwa kishindo Nagoya Marathon

T L