• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
WANTO WARUI: KNEC itatue tatizo la uhamaji wa wanafunzi wa CBC kutoka shule moja hadi nyingine

WANTO WARUI: KNEC itatue tatizo la uhamaji wa wanafunzi wa CBC kutoka shule moja hadi nyingine

NA WANTO WARUI

MFUMO mpya wa elimu unaojulikana kama CBC hatimaye umefikia kilele cha kuwatahini wanafunzi wake wa kwanza mwaka huu ambao ni wale wa Gredi ya 6.

Hata hivyo, mambo bado hayajanyooka kwa kuwa mfumo wenyewe una changamoto kadha wa kadha ambazo zinaukumba.

Moja ya changamoto hizo ni uhamishaji wa wanafunzi hasa wa Gredi ya Nne hadi Sita.

Wanafunzi hawa wanahamishwa kutoka shule moja hadi nyingine kupitia njia ya mtandao unaosimamiwa na Taasisi ya Mitihani Nchini, KNEC.

Licha ya hayo, kuna barua ya uhamisho ambayo inafaa kuchukuliwa katika ofisi za elimu za kaunti ndogo, ipelekwe kujazwa na mwalimu mkuu wa shule ambayo mwanafunzi anahama kisha ijazwe na mwalimu mkuu wa shule inayompokea mwanafunnzi na hatimaye ipelekwe katika ofisi za elimu ambapo mwanafunzi amehamia.

Shughuli ya aina hii ina uchovu mwingi sana na usumbufu hasa tunapokuwa katika nyakati za kiteknolojia.

Kumhamisha mwanafunzi kwa njia ya mtandao kunafaa zaidi kwa kuwa ni rahisi pia ni adhimu kwani KNEC ina uwezo wa kukagua shughuli hizo zote za uhamaji.

Haina maana wazazi kusumbuliwa na vijikaratasi huku wakitembea kilomita nyingi sana kutafuta nakala za uhamisho ilhali inatosha kuhamisha wanafunzi kwa mtandao.

Jambo jingine ni, kuna walimu wengi wakuu ambao ama hawaelewi jinsi ya kuendesha shughuli za kuhamisha wanafunzi mtandaoni au wanapuuza utaratibu ufaao.

Kasoro hii inasababisha mwanafunzi kusajiliwa zaidi ya mara moja hivyo basi kuwa na namba mbili za mtihani kutoka kwa KNEC.

Inapotokea mwanafunzi amehama shule moja akiwa na namba yake ya mtihani kisha shule anayohamia ikakataa kufuata kanuni zilizowekwa za uhamisho na kumpa namba nyingine, basi mwanafunzi huyo atakuwa amepoteza baadhi ya alama zake za mitihani ya awali.

Hivi ni kusema kuwa pendekezo la KNEC la wanafunzi kukaguliwa na kutahiniwa huku wakiendelea kusoma huenda likawa na kasoro nyingi.

KNEC inapendekeza 20% ya alama katika Gredi ya 4, 20% nyingine kutoka Gredi ya 5 na asilimia inayobaki iwe kutoka mtihani wa mwisho wa Gredi ya 6.

Tayari kuna shule nyingi ambazo hazijawasilisha alama hizi huku zikiendelea kuweka wanafunzi na wazazi wasio na ufahamu katika lindi la giza.

Hatua za dharura zinafaa kuchukulia ili kurekebisha makosa haya.

Iwapo kuna wanafunzi walio katika Gredi ya Sita kwa mfano, na alama zao bado hazijawasilishwa kwa KNEC, basi itabidi KNEC na Wizara ya Elimu zitafuta mbinu ya kuhakikisha kuwa wanafunzi ambao hawajajaziwa alama wanashughulikiwa ili kuwaepushia tatizo hilo ambalo linaweza kuathiri masomo yao milele.

  • Tags

You can share this post!

ODM, DAP-K wazozania Nyanza, Magharibi

WANDERI KAMAU: Uchumi: Kuna uwezekano Serikali inawapotosha...

T L