• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:07 PM
ODM, DAP-K wazozania Nyanza, Magharibi

ODM, DAP-K wazozania Nyanza, Magharibi

OKONG’O ODUYA na KASSIM ADISANI

CHAMA cha ODM kinakabiliwa na kibarua kipya katika ngome zake maeneo ya Magharibi na Nyanza, baada ya chama cha Democratic Action Party of Kenya (DAP-K) kusisitiza kuwa kitawasimamisha wagombea wake kushindana na wale wa ODM.

Kuna hofu kuwa mvutano kati ya vyama hivyo viwili, ambavyo ni wanachama wa muungano wa Azimio La Umoja-One Kenya, huenda ukaathiri kampeni za Bw Odinga katika maeneo hayo, Uchaguzi Mkuu wa Agosti unapokaribia.

Vyama hivyo viko kwenye ushindani mkubwa kujizolea ufuasi katika maeneo hayo, huku ODM ikisisitiza kuwa DAP-K haifai kuwasimamisha wawaniaji wake ili kushindana na wale wa ODM.

Katika Kaunti ya Siaya, viongozi wa DAP-K eneo hilo wanasema kuwa ODM haifai kumsimamisha mgombea kwa nafasi ya Useneta.

Badala yake, wanasisitiza kuwa lazima ODM imuunge mkono Bw Oscar Onyango, anayewania nafasi hiyo kwa tiketi ya DAP-K.

Viongozi hao walisema kuwa Bw Onyango ndiye mwaniaji pekee ambaye ni kijana kwenye nafasi hiyo.

Wawaniaji wengine ni Bw Julius Okinda (mwaniaji huru), Bw Tony Yogo (mwaniaji huru) na Dkt Oburu Oginga (ODM).

Mwenyekiti wa DAP-K katika kaunti hiyo, Bw John Aduda, alisema kuwa ikiwa ODM itamuunga mkono mwaniaji huyo, basi hilo litakuwa hakikisho kuwa Bw Odinga atapata uungwaji mkono wa kutosha kwenye azma yake ya kuwania urais.

“DAP-K kilikuwa chama cha kwanza kumuunga mkono Bw Odinga katika eneo la Magharibi kabla ya vyama vingine. Ikiwa ODM itamuunga mkono mwaniaji wetu, Azimio itakuwa maarufu katika kaunti hii (Siaya) na eneo zima la Magharibi,” akasema Bw Aduda.

Akaongeza: “Wawaniaji wa ODM katika nyadhifa mbalimbali za kaunti ni viongozi ambao wamekuwa kwenye ulingo wa siasa kwa muda mrefu. Ili kuruhusu vijana kujijenga kisiasa, ODM inapaswa kumuunga mkono mwaniaji useneta wa DAP-K ambaye ni kijana.”

ODM huwa ina ufuasi mkubwa katika kaunti hiyo.

Bw Onyango alisema kuwa yuko tayari kushirikiana na ODM kuhakikisha kuwa Bw Odinga amepata uungwaji mkono wa kutosha katika kaunti hiyo.

“Lengo kuu ni kuhakikisha Bw Odinga amechaguliwa kuwa rais wa tano wa Kenya. Tayari tushanyakua nyadhifa nyingine. Hivyo, ikiwa ODM itaniunga mkono kuwania useneta, hilo litatoa nafasi kwa kila chama katika Azimio kupata mgao wa nyadhifa hizo katika eneo la Magharibi,” akasema Bw Onyango.

  • Tags

You can share this post!

Shiney apiga abautani akiweka zingatio kwa muziki wa Injili

WANTO WARUI: KNEC itatue tatizo la uhamaji wa wanafunzi wa...

T L