• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 7:50 AM
WANTO WARUI: Serikali za kaunti zisaidie wanafunzi wanaokosa masomo kutokana na njaa

WANTO WARUI: Serikali za kaunti zisaidie wanafunzi wanaokosa masomo kutokana na njaa

NA WANTO WARUI

HUKU janga la njaa likiendelea kuathiri maelfu ya Wakenya, idadi ya wanafunzi wanaokosa masomo inaendelea kuongezeka kila siku.

Watu wapatao 3.5 milioni katika zaidi ya kaunti ishirini nchini hawana chakula kamwe. Kaunti za kaskazini mwa Kenya kama vile Marsabit, Mandera, Wajir, Turkana na nyinginezo ndizo zilizoathirika pakubwa.

Kuna zaidi ya wanafunzi 160,000 kote nchini ambao wameacha kwenda shuleni kwa sababu ya makali ya njaa.

Idadi hii ni kubwa mno na inaendelea kuongezeka kila siku. Mpango uliokuwapo awali wa kuwapa wanafunzi chakula hasa wale wa shule za msingi ulikuwa ukisaidia sana na ingekuwa bora iwapo ungerudishwa.

Pamoja na hayo, serikali za kaunti zinafaa kuwajibika na kuingilia kati ili kusaidia wanafunzi ambao wameathiriwa na janga hili katika kaunti zao. Ikiwa mipango maalum inaweza kufanywa katika mabunge ya kaunti, wawakilishi wa wodi wanaweza kupitisha bajezi za dharura kusaidia wanafunzi wasioenda shuleni ili waweze kusoma.

Aidha, serikali zizo hizo kwa ushirikiano na serikali kuu zinafaa kuanzisha mpango maalum ambao utasimamia utoaji chakula cha mchana kwa wanafunzi shuleni ili kuepuka tatizo kama hili kujirudia mara kwa mara.

Serikali kuu nayo itoe fedha za maendeleo ya kaunti bila kuchelewesha ili kaunti ziweze kujipanga ipasavyo kwa wakati. Endapo tutawaachia tu wadhamini na wahisani kutoa misaada, wanafunzi wetu hawataweza kupata masomo kwani wahisani hawa wanatoa misaada ya siku chache tu isiyoweza kutosheleza mahitaji ya wanafunzi. Hata hivyo, juhudi za wahisani hawa za kutoa misaada ni muhimu sana na zinaungwa mkono na kila Mkenya.

Wizara ya elimu pia izingumzie kuhusu janga hili.

  • Tags

You can share this post!

Wanasiasa kuvuna kwa uaminifu wao

MWALIMU WA WIKI: Vienna si bora tu, ni mwalimu bora

T L