• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 1:56 PM
Wanasiasa kuvuna kwa uaminifu wao

Wanasiasa kuvuna kwa uaminifu wao

NA BENSON MATHEKA

KUBADILISHWA kwa orodha ya watakaohojiwa kwa nyadhifa za makatibu wa wizara kumeonyesha kwamba kigezo kikuu cha kuhudumu katika serikali ya Kenya Kwanza kitakuwa uaminifu kwa Rais William Ruto na kwa ajenda zake.

Ingawa wataalamu wa utawala wanasema kwamba viongozi wengi huteua watu waaminifu kwao katika serikali zao, makatibu wa wizara hawafai kuwa wanasiasa inavyoweza kufanyika katika serikali ya Kenya Kwanza.

Rais Ruto amependekeza wanasiasa waliomuunga mkono wakati alipoanza kampeni za uchaguzi mkuu uliopita kuwa mawaziri katika serikali yake, hali ambayo inaweza kujirudia katika uteuzi wa makatibu wa wizara.

Kulingana na Tume ya Utumishi wa Umma (PSC), Wakenya 9,000 walituma maombi ya nyadhifa za makatibu wa wizara.

Hata hivyo, orodha ya kwanza iliyotolewa Alhamisi ilikuwa na majina 477 kabla ya kubadilishwa Ijumaa na kuchapishwa upya ikiwa na majina 585.

Miongoni mwa 108 walioongezwa katika orodha hiyo mpya ni washirika na washauri wa Rais Ruto na viongozi wa vyama tanzu vya muungano wa Kenya Kwanza, ishara kwamba makatibu wa wizara waliohudumu katika serikali zilizotangulia huenda wakaondolewa.

Miongoni mwa waliokuwa wameachwa nchi katika orodha ya kwanza iliyotolewa Alhamisi ni wanasiasa wa muungano wa Kenya Kwanza walioshindwa kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9 na wataalamu waliochangia ushindi wa Dkt Ruto.

Katika kile kinachoonekana kama juhudi za kuzawidi washirika wake kwa kumsaidia katika kampeni, Rais Ruto ameongeza idadi ya makatibu wa wizara kutoka 44 hadi 49.

Orodha hiyo imejaa wanasiasa na watu walio na uhusiano na Kenya Kwanza.

Aliyekuwa seneta maalum Isaac Mwaura aliyewania ubunge wa Ruiru kwa tikiti ya chama cha UDA yuko katika orodha hiyo sawa na mtaalamu wa uchumi Moses Banda Mwendwa aliyekuwa katika kamati ya kitaifa ya kampeni za Rais Ruto.

Wengine ni aliyekuwa mbunge wa Lang’ata Nixon Korir aliyekuwa mstari wa mbele katika kampeni za Kenya Kwanza, aliyekuwa mbunge maalum David Ole Sankok pia limeongezwa katika orodha hiyo. Bw Sankok alikuwa mtetezi mkubwa wa Dkt Ruto tangu 2018 alipotengwa na chama cha Jubilee.

Wakili Alutalala Moses Mukhwana ambaye ni mshauri wa masuala ya kisheria wa kiongozi wa ANC, Musalia Mudavadi, na kamishna wa Tume ya Uchaguzi (IEBC) Boya Molu pia waliorodheshwa.

Aliyekuwa shahidi wa Dkt Ruto katika kesi ya kupinga matokeo ya urais katika Mahakama ya Upeo, Bw Raymond Kiprotich Bett pia aliongezwa katika orodha hiyo.

Prof Julius Bitok aliyekuwa balozi wa Kenya nchini Pakistan na mshirika wa karibu wa Dkt Ruto, aliyekuwa mbunge wa Kinango Benjamin Tayari, aliyekuwa mbunge wa Magarini Michael Kingi, Ali Menza Mbogo (aliyekuwa mbunge wa Kisauni), Francis Kariuki Mugo (aliyewania useneta wa Lamu kupitia UDA), Lung’anzi Chai Mangale (aliyewania ugavana Kwale kupitia PAA), Jimmy Kahindi (aliyekuwa spika wa bunge la Kilifi) na baadhi yao.

Wengine ni aliyekuwa gavana wa Samburu, Moses Lenolkulal ambaye Dkt Ruto alimshawishi asitetee kiti chake kwenye mchujo wa UDA mwezi Aprili na aliyekuwa naibu gavana wa Kisii, Joash Maangi pia wanamezea mate nyadhifa hizo.

Mshirika wa Dkt Ruto kutoka eneo la Ukambani, Jonathan Mueke pia ameorodheshwa kuhojiwa.

Duru ndani ya Kenya Kwanza zinasema kwamba baadhi ya waliokuwa wameachwa nje kwenye orodha hiyo ni watu ambao Dkt Ruto aliahidi kazi kwa uaminifu wao kwake, na kulingana na makubaliano yake na viongozi wa vyama tanzu.

  • Tags

You can share this post!

Afisa ashauri wakazi kuwekeza kwa ufugaji samaki ili...

WANTO WARUI: Serikali za kaunti zisaidie wanafunzi...

T L