• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
MWALIMU WA WIKI: Vienna si bora tu, ni mwalimu bora

MWALIMU WA WIKI: Vienna si bora tu, ni mwalimu bora

NA CHRIS ADUNGO

UKIITIKIA wito wa kuwa mwalimu, fahamu kwamba taifa lote la kesho linakutegemea.

Jamii nzima huwa imekuamini na mtoto ambaye mzazi wake amekuachia shuleni. Kwa sababu hiyo, matarajio ya kila mtu kwako huwa ni ya kiwango cha juu sana.

Falsafa hii imekuwa mwongozo madhubuti kwa mwalimu Vienna Wanaswa ambaye sasa anafundisha Kiswahili na Dini katika shule ya Newlight iliyoko Kitengela, Kaunti ya Kajiado.

Kwa mtazamo wake, yeyote asiyeweza kuwajibika na kujituma ipasavyo kiasi cha kusalia na mwanafunzi ubavuni pake kila wakati, basi hafai kabisa kujitosa katika ulingo wa ualimu.

Vienna anashikilia kuwa, wanafunzi humwamini sana mwalimu aliye na ufahamu mpana wa masomo anayofundisha. Hivyo, mwalimu bora anastahili kufanya utafiti wa kina katika somo lake na kuchangamkia vilivyo masuala yote yanayofungamana na mtaala.

“Anapaswa pia kuelewa uwezo, changamoto na mahitaji ya msingi ya kila mwanafunzi. Ajitahidi kuhudhuria vipindi vyote, atoe mazoezi ya kutosha kwa wanafunzi, arejeshe masahihisho ya kazi mapema na awape wanafunzi matokeo ya majaribio ya mitihani kwa wakati unaofaa,” anasema.

“Mbali na kuwa mnyumbufu wakati wa kuandaa vipindi vya somo lake na mbunifu katika uwasilishaji wa kile anachokifundisha, inampasa pia awe na ujuzi wa kutumia nyenzo anuwai za ufundishaji zitakazowaamshia wanafunzi ari ya kuthamini masomo,” anaelezea.

Vienna alizaliwa katika eneo la Sirisia, Kaunti ya Bungoma. Ndiye mwanambee katika familia ya watoto wanne wa Bw Wanaswa Njalale na Bi Betina Makhanu Wanyama.Alisomea katika shule za msingi za Kibabii (2005-2010) na Nzoia Sugar Company (2011-2012) zilizoko Bungoma kabla ya kujiunga na shule ya upili ya St Brigid’s Girls Kiminini, Kaunti ya Trans-Nzoia (2013-2016).

Japo matamanio yake yalikuwa kujitosa katika taaluma ya udaktari, alihiari kusomea ualimu (Kiswahili/Dini) katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU) kati ya 2017 na 2020.Uamuzi wa kujibwaga katika ulingo wa ualimu yalikuwa zao la kuchochewa zaidi na Bw David Kamau na Bi Henrica Wanyonyi waliompokeza malezi bora ya kiakademia katika shule ya upili.

Vienna alipokea mafunzo ya nyanjani katika shule ya St Mary’s Kibabii mwaka wa 2020 na akaajiriwa na Newlight Schools mnamo Agosti 2021. Kubwa zaidi katika maazimio yake ni kujiendeleza kitaaluma kwa lengo la kuweka hai ndoto za kuwa profesa wa Kiswahili na mhadhiri wa chuo kikuu.

Zaidi ya ualimu, Vienna ni mwanamitindo wa fasheni za Kiafrika. Anapania pia kuzamia kikamilifu katika uandishi wa fasihi ili kuendeleza kipaji cha utunzi wa kazi bunilizi kilichoanza kujikuza ndani yake utotoni.

Alichapishiwa ‘Mwongozo wa Tamthilia ya Bembea ya Maisha’ (Timothy Arege) mnamo Agosti 2022.

  • Tags

You can share this post!

WANTO WARUI: Serikali za kaunti zisaidie wanafunzi...

Urusi yaimarisha ulinzi katika daraja la Crimea

T L