• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 5:01 PM
AFC Leopards kutema wachezaji kadhaa kabla ya msimu mpya

AFC Leopards kutema wachezaji kadhaa kabla ya msimu mpya

NA JOHN ASHIHUNDU

AFC Leopards imepania kukisuka upya kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao wa 2023/2024, huku swala la kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Kenya (FKF) likipewa kipaumbele.

Habari za kuaminika zimedai kwamba tayari klabu hiyo kongwe imetambua wachezaji kadhaa wapya wanaotarajiwa kukiongezea nguvu kikosi hicho cha kocha Patrick Aussems.

Kulingana na duru hizo, wachezaji kadhaa watafungishwa virago, huku wengine chipukizi wakitumwa kwa mkopo kuchezea timu nyingine ili wajinoe zaidi.

Wachezaji wanne wamepangiwa kuachiliwa wajiunga na timu nyingine baada ya viwango vyao kutoridhisha idara ya kiufundi.

Kulingana na habari kutoka afisi kuu ya klabu hiyo, beki Collins Shivachi, mlinzi Tedian Esiliba na aliyekuwa beki wa kushoto wa Wazito FC Washington Munene na Musa Saad ambaye ni raia wa Sudan Kusini, ni miongoni mwa wanaotarajiwa kuachiliwa.

Esilaba amecheza mechi chache kutokana na majeraha ya mara kwa mara, na huenda klabu hiyo imeonelea mchango wake ulikuwa mdogo tangu ajiunge na klabu hiyo mnamo 2021 akitokea Nairobi City Stars. Shivachi na Saad wamekuwa wakitokea kwenye benchi.

Kipa chipukizi Maxwell Mulili, Loren James, Nesta Olum, Njite Ochieng, Giovanni Lukhumwa, Owen Mboya, Maxwell Otieno na Daniel Sunguti ambao walijiunga na kikosi kikuu wakitokea timu B wataachiliwa kwa mkopo.

Habari zimesema Ingwe imevamia nyota kadhaa kutoka klabu ya Nzoia Sugar ambao ni miongoni mwa walio kwenye orodha ya wanaolengwa kusaini mikataba. Nyota hao ni pamoja na Kipa Humphrey Katasi, Kevin Juma, kiungo mahiri Beja Hassan, Bonface Munyendo na mshambuliaji matata Joseph Mwangi.

Vile vile Leopards wanawinda mlinzi wa katikati, Gedion Were kutoka Mathare United, Nashon Alembi na mshambuliaji John Avire ambaye hana klabu kwa sasa. Kadhalika Ingwe inammezea mate mshambuliaji chipukizi Beja Nyamawi wa SS Assad ya Supa Ligi (NSL).

Wakati huo huo, kocha wa Nzoia Sugar, Salim Babu amesema licha ya uvumi kwamba wachezaji wake kadhaa wataondoka, kikosi chake kitabakia imara kwa msimu ujao.

Klabu hiyo kutoka Kaunti ya Bungoma imekuwa miongoni mwa tatu bora ligini, ikifukuzana vikali na Gor Mahia na Tusker jedwalini.

“Hata kama wataondoka, kuna wachezaji wengi nchini ambao nitasajili kujaza nafasi za watakaoondoka. Nina mwaka mmoja kwenye mkataba wangu na ningali hapa kuendelea kutekeleza wajibu wangu,” Babu akasema.

Nzoia wanakamata nafasi ya tatu kwa alama 63, pointi nne tu nyuma ya vinara Gor Mahia, wakati Tusker wakiwapitia pointi mbili pekee.

Mnamo Jumatano, wamepangiwa kucheza na Kenya Commercial Bank (KCB) kabla ya kumalizana na Sofapaka katika mechi zao zilizobakia.

  • Tags

You can share this post!

Miili miwili zaidi yatolewa kwenye vifusi vya ghorofa...

Diwani ataka vijana waliookoa maisha ya wengi jumba...

T L