• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
AFC yaibebesha Talanta mabao, Posta Rangers na Wazito zikitoka sare

AFC yaibebesha Talanta mabao, Posta Rangers na Wazito zikitoka sare

JOHN ASHIHUNDU Na CECIL ODONGO

AFC Leopards jana Alhamisi ilisajili ushindi mkubwa katika Ligi Kuu (KPL) msimu huu baada ya kuikomoa FC Talanta 6-0 katika uwanja wa Kasarani.

Kwenye uga jirani wa Kasarani Annex, Posta Rangers waliagana sare ya 1-1 na Wazito.

Mvamizi mahiri Victor Omune alifunga mabao manne huku Cliff Nyakeya akicheka na nyavu mara mbili na kuivunia Ingwe ushindi huo mkubwa.

Katika mechi ya pili Collins Neto alitoka kwenye benchi na kufunga kipindi cha pili bao ambalo lilifuta lile la Posta Rangers lililokuwa limefungwa na Sammy Odero.

Ushindi dhidi ya FC Talanta uliisukuma Ingwe hadi nafasi ya tano kwa alama 25 sawa na Tusker ambayo inadunishwa na uchache wa mabao.

Ingwe imecheza mechi 15 huku Wanamvinyo hao wakijibwaga uwanjani mara 14.

FC Talanta ambayo inaandamwa na changamoto za kifedha nayo ipo nambari 14 kwa alama 12 baada ya mechi 14.
Sare dhidi ya Wazito inaiweka Posta Rangers katika nafasi ya 11 kwa alama 18 kutokana na mechi 15.

Wazito nao wapo pabaya kwa kuwa wana alama tisa baada ya kujibwaga uwanjani mara 12.

Baada ya kisa cha wiki jana ambapo Kocha wa AFC Leopard Patrick Aussems alikashifiwa kwa kumtusi mwanahabari, jana aliamua kuyajibu maswali yao kwa Kifaransa na kuwaacha wasiofahamu lugha hiyo kujikuna kichwa huku wakizubaa na kujiuliza wamefanya nini.

Baada ya mahojiano hayo wanahabari wengi waliulizana ‘amesema nini’ wakibaki na kujiendea.

Kocha wa FC Talanta alisema kuwa tatizo ni wachezaji kutolipwa kwa zaidi ya mwaka mmoja.

“Hatuna uwanja wa kufanyia mazoezi na hatujalipwa kwa zaidi ya mwaka mmoja. Hatuna msaada wowote na hata dhidi ya Wazito nilitumia pesa yangu kusafirisha timu hiyo hadi Muhoroni,” akasema Kenyatta.

Aliongeza kuwa kwa sasa hali ni ngumu ndani ya timu hiyo na wachezaji hawana motisha huku wadhamini wa FC Talanta ambao ni Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (CAK) wakitokomea.

Mshambuliaji wa timu hiyo Brian Yakhama na kipa Kevin Otieno walipata jeraha na walikosa mechi hiyo licha ya kuwa wao ni wachezaji tegemeo.

  • Tags

You can share this post!

DOMO: Sanaa ya injili ya Kenya hakika imejaa vibonzo

Utamaduni tata wa ‘Tero Buru’ katika mazishi ya...

T L