• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:46 PM
AFCON: Mali yapiga Tunisia katika mchuano wa Kundi F uliokamilika kwa vituko vya refa

AFCON: Mali yapiga Tunisia katika mchuano wa Kundi F uliokamilika kwa vituko vya refa

Na MASHIRIKA

MALI walitandika Tunisia 1-0 katika mechi ya Kundi F kwenye fainali za Kombe la Afrika (AFCON) nchini Cameroon.

Hata hivyo, mchuano huo ulitamatika kwa utata mwingi baada ya refa raia wa Zambia, Janny Sikazwe kupuliza kipenga cha mwisho kabla ya dakika 90 kukamilika.

Kocha Mondher Kebaier wa Carthage Eagles ya Tunisia aliongoza benchi yake ya kiufundi kujitoma uwanjani kumkabili Sikazwe aliyepuliza kipenga cha kuashiria mwisho wa mchuano katika dakika ya 85.

Baada ya vinara wa timu zote husika na waandalizi wa mechi kushauriana, iliamuliwa wachezaji warudi uwanjani kutandaza soka kwa dakika tano zilizosalia.

Hata hivyo, wachezaji wa Tunisia walikataa kurejea uwanjani na Mali wakaibuka washindi wa gozi hilo.

Wasimamizi wa mechi hiyo walisindikizwa nje ya uwanja na idadi kubwa ya maafisa wa usalama huku wachezaji wa Mali wakisherehekea mbele ya mashabiki wao.

Bao la pekee na la ushindi kwa upande wa Mali lilifumwa wavuni na Ibrahima Kone kupitia penalti ya dakika ya 48. Mkwaju huo ulitokana na tukio la Ellyes Skhiri kunawa mpira ndani ya kijisanduku.

Ingawa Tunisia nao walipata penalti katika dakika ya 77, mkwaju ambao mabingwa hao wa AFCON 2004 walipigiwa na Wahbi Khazri ulipanguliwa na kipa wa Mali, Ibrahim Mounkoro.

Mali walikamilisha mechi wakiwa na wachezaji 10 pekee uwanjani baada ya El Bilal Toure kuonyeshwa kadi nyekundu mwishoni mwa kipindi cha pili baada ya kumchezea visivyo Dylan Bronn.

Japo Mali si miongoni mwa vikosi vinavyopigiwa upatu wa kutwaa taji la AFCON mwaka huu, kikosi hicho kinajivunia rekodi ya kutopigwa hadi kufikia sasa katika mechi yoyote ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Natembeya ajitunuka sifa akisimulia jinsi alivyokabili...

Gakuyo ahimiza wafuasi wake wafuate ngoma ya Azimio la Umoja

T L