• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:46 PM
Natembeya ajitunuka sifa akisimulia jinsi alivyokabili Mungiki

Natembeya ajitunuka sifa akisimulia jinsi alivyokabili Mungiki

Na SAMMY WAWERU

MSHIRIKISHI Mkuu wa Bonde la Ufa anayeondoka, Bw George Natembeya amejisifu kwa rekodi yake ya utendakazi akiwa mtumishi wa umma akisema imempa msukumo wa kujitosa katika ulingo wa siasa.

Akizungumza Jumatano jijini Nakuru alipotangaza rasmi nia yake kuwania kiti cha ugavana Trans Nzoia, Bw Natembeya alirejelea jitihada za utendakazi wake akiwa Mkuu wa Wilaya (DC) ya Murang’a 2007.

Alisema ni kupitia ukakamavu wake kukabiliana na uhalifu, alifanikiwa kuzima kundi haramu la Mungiki.

“Nilipopata uhamisho kuhudumu Murang’a, niliapa kati yangu (George Natembeya) na vuguvugu haramu la Mungiki kuna yule ataacha alichokuwa akifanya.

“Hatimaye mmoja wetu alilazimika kusaliti amri, na si mimi. Hata nyinyi mnaweza kujijazia ni nani aliinua mikono,” Bw Natembeya akaambia wanahabari, akikumbusha alivyoongoza oparesheni kufurusha kundi hilo.

Vuguvugu hilo likitajwa kuhangaisha wananchi hasa eneo la Mlima Kenya na Nairobi, wanachama wake walikuwa wakitwaa biashara za watu – kutoza ada na hata kuua kinyama kwa waliokaidi amri.

Aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Bw John Michuki japo kwa sasa ni marehemu, alitangaza Mungiki kuwa haramu akiamuru maafisa wa usalama kupiga risasi washirika wanapoonekana wakihusika uhalifu.

Akitangaza kujiuzulu kama Mshirikishi Mkuu Bonde la Ufa, Natembeya alisema wito kujitoma kwa siasa ulitokana na wakazi wa Kaunti ya Trans Nzoia akisema “wamenihimiza kuwa gavana wao 2022 ili kuboresha maisha yao”.

Alipohamishiwa Nairobi, eneo la Kamukunji kutoka Murang’a, Bw Natembeya anasema aliweza kutimua wanamgambo wa Al-Shabaab chini ya siku 100 za usimamizi wake.

Akihudumu kama Kamishna Kaunti ya Narok, alikalia ngumu mtandao wa wahuni wanaoendeleza upashaji tohara kwa wasichana na wanawake (FGM) na ndoa za mapema.

Aidha, anakumbukwa kutokana na tangazo lake wanafunzi wa kike Narok wafanyiwe uchunguzi endapo wamepashwa tohara na vipimo vya ujauzito kabla kuruhusiwa kurejea shuleni baada ya likizo.

Baadhi ya mashirika kutetea haki za kibinadamu na wadau katika sekta ya elimu walikosoa msimamo huo, wakiutaja kama uliovuka mipaka ya siri za wasichana

Bw Natembeya hata hivyo hakulegeza kamba, akiwataka machifu kuhakikisha FGM inakabiliwa vilivyo na wanaume wahuni wanaotunga mimba wasichana wa shule kuadhibiwa vikali kisheria.

Mwaka wa 2015, Bw Natembeya alihudumu kama Kamishna Kaunti ya Isiolo ambapo aliagiza maafisa wa polisi kupiga risasi wanaomiliki bunduki na silaha hatari kinyume cha sheria katika oparesheni aliyoongoza kukabiliana na wizi wa mifugo.

Mnamo Jumatano hata hivyo akitoa tangazo kuwania ugavana Trans Nzoia, alisema utovu wa usalama na wizi wa mifugo Kerio Valley ungali kero.

  • Tags

You can share this post!

Staa wa Bandari FC Shaaban Kenga kurudi uwanjani

AFCON: Mali yapiga Tunisia katika mchuano wa Kundi F...

T L