• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Agala na Makokha wabanduliwa kwenye voliboli ya ufukweni Tokyo

Agala na Makokha wabanduliwa kwenye voliboli ya ufukweni Tokyo

Na GEOFFREY ANENE

WAKENYA Brackcides Agala na Gaudencia Makokha wamekubali kipigo cha pili mfululizo katika voliboli ya ufukweni, Kundi D, kwenye Olimpiki 2020 baada ya kupondwa na Amerika kwa seti 2-0 jijini Tokyo, Japan hapo Alhamisi.

Wawili hao, ambao wanaorodheshwa nafasi ya 97 duniani, hawakuwa na lao walipokutana na nambari tatu duniani Kelly Claes/ Sarah Sponcil na kupoteza bila hata ya kufikisha alama 10. Walilemewa katika seti hizo kwa alama 21-8, 21-6.

Agala na Makokha waliingia mechi hiyo baada ya kufungua kampeni yao kwa kupoteza kwa seti 2-0 za alama 21-15, 21-9 mikononi mwa Wabrazil Ana Patricia na Rebecca mnamo Julai 26.

Mechi ya mwisho ya Wakenya hao itakuwa dhidi ya raia wa Latvia Anastasija Kravcenoka/Tina Graudina (nambari 17 duniani) hapo Julai 31.

Claes/Sponcil wanaongoza kundi hilo kwa alama nne kutokana na kupiga pia Graudina/Kravcenoka 2-1.

Timu ya Patricia/Rebecca na Graudina/Kravcenoka zimezoa alama tatu kila moja nayo Kenya ina alama mbili. Kuna makundi sita ya timu nne kila moja. Timu tatu bora kutoka kila kundi zitajikatia tiketi ya raundi ya 16-bora. Kulishwa vichapo viwili mfululizo kunamaanisha kuwa Kenya haiwezi kuingia raundi ya 16-bora.

You can share this post!

AKILIMALI: Kujiamini kumemfanya awe hodari katika...

Kigogo Novak Djokovic ampepeta Nishikori na kutinga...