• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Kigogo Novak Djokovic ampepeta Nishikori na kutinga nusu-fainali za tenisi ya mchezaji mmoja kila upande kwenye Olimpiki

Kigogo Novak Djokovic ampepeta Nishikori na kutinga nusu-fainali za tenisi ya mchezaji mmoja kila upande kwenye Olimpiki

Na MASHIRIKA

NOVAK Djokovic wa Serbia sasa yuko pazuri zaidi kutia kapuni dhahabu ya Olimpiki baada ya kumdengua Kei Nishikori wa Japan na kutinga nusu-fainali za mchezaji mmoja kila upande.

Nyota huyo anayeorodheshwa wa kwanza duniani, anapania kuwa mwanamume wa kwanza kunyankua mataji yote manne ya Grand Slam pamoja na dhahabu ya Olimpiki katika kipindi cha mwaka mmoja.

Alimpokeza Nishikori kichapo cha 6-2, 6-0 na kujikatia tiketi ya kumenyana na ama Alexander Zverev wa Ujerumani au Jeremy Chardy wa Ufaransa kwenye hatua ya nusu-fainali.

Awali, Belinda Bencic wa Uswisi alikuwa amemzaba Elena Rybakina wa Kazakhstan 7-6 (7-2) 4-6 6-3 na kutinga fainali ya tenisi ya wanawake kwa mchezaji mmoja mmoja kila upande.

Bencic atavaana sasa na mshindi wa nusu-fainali ya pili kati ya Elina Svitolina wa Ukraine na Marketa Vondrousova wa Jamhuri ya Czech.

Bencic, 24, alimpiku Rybakina katika mchezo ambao mshindi aliamuliwa baada ya seti tano zilichukua kipindi cha saa tano.

Kwa upande wake, Djokovic alihitaji saa moja na dakika 10 pekee kumbwaga Nishikori aliyezolea Japan nishani ya shaba mnamo 2016 kwenye Olimpiki za Rio de Janeiro, Brazil.

Ushindi wa Djokovic ulimwezesha kufikia rekodi ya Roger Federer na Rafael Nadal aliyejizolea nishani ya 20 ya Grand Slam kwenye kivumbi cha Wimbledon mnamo Juni 2021. Watatu hao sasa wanajivunia rekodi ya kushinda jumla ya michuano 13 ya tenisi ya mchezaji mmoja kila upande kwenye Olimpiki.

Hata hivyo, Djokovic hajawahi kutinga fainali ya Olimpiki huku matokeo bora zaidi aliyowahi kusajili kwenye michezo hiyo yakiwa ni kuzoa nishani ya shaba baada ya kupigwa na Nadal mnamo 2008 jijini Beijing, China.

Pablo Carreno Busta wa Uhispania atakutana na Karen Khachanov wa Urusi kwenye nusu-fainali nyingine itakayotandazwa Ijumaa ya Julai 30, 2021 katika ukumbi wa Ariake Tennis Park.

Mhispania huyo alimduwaza Daniil Medvedev anayeorodheshwa wa pili duniani kwa kichapo cha 6-2 7-6 (7-5) huku Khachanov akimlaza Ugo Humbert wa Ufaransa kwa 7-6 (7-4) 4-6 6-3.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Agala na Makokha wabanduliwa kwenye voliboli ya ufukweni...

China yavunja rekodi ya dunia kwenye uogeleaji wa 4x200m...