• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 4:40 PM
Aguero kuagana rasmi na Man-City mwishoni mwa msimu

Aguero kuagana rasmi na Man-City mwishoni mwa msimu

Na MASHIRIKA

MFUNGAJI bora wa muda wote kambini mwa Manchester City, Sergio Aguero, ataagana rasmi na kikosi hicho mwishoni mwa msimu huu wa 2020-21.

Mkataba wa sasa kati ya Man-City na Aguero, 32, unakamilika rasmi mwishoni mwa muhula huu na waajiri wake wamemweleza kwamba hautarefushwa.

Nyota huyo raia wa Argentina alijiunga na Man-City mnamo 2011 baada ya kuagana na Atletico Madrid ya Uhispania. Kufikia sasa, amefungia Man-City jumla ya mabao 257 kutokana na mechi 384.

“Kutokana na uelekezi wa wamiliki wa Man-City pamoja na mchango wa wachezaji wengi wengine, tulifaulu kuwa miongoni mwa klabu bora duniani,” akasema Aguero.

Aguero atastahiwa uwanjani Etihad kwa kujengewa mnara kwa pamoja na aliyekuwa nahodha wa Man-City Vincent Kompany na kiungo wa zamani wa kikosi hicho, David Silva. Kompany na Silva waliagana na Man-City mnamo 2019 na 2020 mtawalia.

Watatu hao walikuwa na mchango mkubwa kambini mwa Man-City huku Aguero akifunga bao la dakika ya mwisho dhidi ya Queens Park Rangers (QPR) mnamo 2012 na kunyanyulia miamba hao taji lao la kwanza la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kipindi cha miaka 44.

Tangu wakati huo, Aguero amesaidia Man-City kutia kapuni mataji matatu zaidi ya EPL, moja la Kombe la FA na matano ya League Cup.

“Mchango wa Aguero kambini mwetu chini ya kipindi cha miaka 10 iliyopita hauwezi kuelezeka. Yeye ni nguli wetu na kumbukumbu zake zitaishi katika mioyo ya wote wanaopenda soka na wanaostahi klabu ya Man-City,” akasema mwenyekiti wa kikosi hicho, Khaldoon Al Mubarak.

Aguero hajakuwa tegemeo kubwa la Man-City msimu huu kutokana na wingi wa majeraha ambayo yamemweka mkekani. Hata hivyo, Man-City wangali wanafukuzia jumla ya mataji manne muhula huu – EPL, Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), Kombe la FA na League Cup.

Kutokana na mechi 14 ambazo amesakatia Man-City msimu huu, ameanza mara tisa pekee akiwa mchezaji wa kikosi cha kwanza na amefunga jumla ya mabao matatu.

Hata hivyo, maamuzi ya Man-City kumwachilia Aguero yamekosolewa pakubwa na beki wa zamani wa kikosi hicho, Micah Richards alikuwa sehemu ya timu iliyotwalia Man-City taji la kwanza la EPL mnamo 2011-12.

“Labda ukiwa na mpango wa kujinasia huduma za wavamizi Kylian Mbappe, Erling Braut Haaland au Harry Kane ndipo ushawishike kukatiza uhusiano na Aguero ambaye nahisi angali na mchango mkubwa kikosini,” akasema Richards.

Mbali na miamba wa soka nchini Uhispania, Barcelona, vikosi vingine vinavyowania huduma za Aguero ni Paris Saint-Germain (PSG), Juventus, Chelsea na Inter Milan.

Aguero ndiye wa nne kwenye orodha ya wafungaji bora wa muda wote katika soka ya EPL. Mabao 181 anayojivunia kufikia sasa yanamweka nyuamya Alan Shearer (260), Wayne Rooney (208) na Andrew Cole (187).

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Obado afufua mashambulizi dhidi ya Raila

Ujerumani, Italia na Uswidi watamba katika mechi zao za...