• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:47 PM
KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Argentina roho juu wakishuka dimbani kuvaana na Saudi Arabia katika Kundi C

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Argentina roho juu wakishuka dimbani kuvaana na Saudi Arabia katika Kundi C

Na MASHIRIKA

NYOTA Lionel Messi ataongoza Argentina kupepetana na Saudi Arabia katika mechi ya Kundi C ugani Lusail Iconic.

Mabingwa hao mara mbili wa dunia (1978, 1986) wanapigiwa upatu wa kutamalaki kundi hilo linalojumuisha pia Mexico na Poland watakaomenyana baadaye katika uga wa 974 Stadium jijini Doha mnamo Novemba 22.

Tangu wapokee kichapo cha 2-0 kutoka kwa Brazil katika fainali ya Copa America 2019, Argentina hawajapoteza mechi 36 mfululizo. Miamba hao wanaonolewa na kocha Lionel Scaloni waling’olewa kwenye hatua ya 16-bora ya Kombe la Dunia 2018, miaka minne baada ya Ujerumani kuwapepeta 1-0 katika fainali nchini Brazil.

Saudi Arabia walifungua makala ya 21 ya Kombe la Dunia kwa kichapo kinono cha 5-0 kutoka kwa wenyeji Urusi mnamo 2018.

Argentina wanaoorodheshwa wa tatu kimataifa, wanapigiwa upatu wa kunyanyua Kombe la Dunia mwaka huu nchini Qatar. Mbali na Saudi Arabia (51), washindani wengine wa Argentina katika Kundi C ni Mexico (13) na Poland (26).

Fainali za Kombe la Dunia mwaka huu ni za 18 kwa Argentina kushiriki huku Mexico, Saudi Arabia na Poland watakaomtegemea Robert Lewandowski wa Barcelona wakinogesha kivumbi hicho kwa mara ya 17, sita na tisa mtawalia.

Kombe la Dunia ndilo taji la pekee ambalo Messi hajawahi kunyanyua katika taaluma yake ya usogora. Mfumaji huyo matata wa Paris Saint-Germain (PSG) anatazamiwa kushirikiana vilivyo na masogora wengine wanne wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) – Emiliano Martinez, Christian Romero, Lisandro Martinez na Alexis Mac Allister – ili kutambisha Argentina.

Fainali za mwaka huu ni za tano kwa Messi na za mwisho kwa nyota huyo akivalia jezi za Argentina walionyanyua taji la Copa America kwa mara ya kwanza tangu 1993 mnamo Julai 2021 na kujikatia tiketi ya kuelekea Qatar bila kushindwa kwenye michuano ya mchujo.

Chini ya Scaloni, Argentina wanajivunia mseto wa chipukizi na wanasoka wazoefu kama vile Messi, 35 na Angel di Maria, 34 ambao watashirikiana vilivyo na Paulo Dybala, Julian Alvarez na Lautaro Martinez katika safu ya mbele.

Miamba hao waliambulia nafasi ya pili kwenye Kombe la Dunia mnamo 1990 na 2014 nchini Italia na Brazil mtawalia.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Mabingwa watetezi Ufaransa...

MKU yatoa chakula cha msaada na bidhaa nyingine muhimu Kitui

T L