• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Mabingwa watetezi Ufaransa kuendea ushindi dhidi ya Australia katika Kundi D ili kuepuka mkosi wa mwaka 2002

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Mabingwa watetezi Ufaransa kuendea ushindi dhidi ya Australia katika Kundi D ili kuepuka mkosi wa mwaka 2002

Na MASHIRIKA

LES Bleus wa Ufaransa watashuka uwanjani Al Janoub wakilenga kuzamisha chombo cha Australia katika Kundi D na kuweka hai matumaini ya kuwa kikosi cha tatu baada ya Brazil na Italia kuwahi kunyanyua Kombe la Dunia mara mbili mfululizo.

Hata hivyo, majeraha ambayo yameweka nyota Karim Benzema, N’Golo Kante, Paul Pogba, Christopher Nkunku na Presnel Kimpembe nje ya kikosi cha Ufaransa yanatarajiwa kuchochea zaidi motisha ya Australia wanaolenga kupiga hatua zaidi kwenye fainali za mwaka huu.

Australia wanaoorodheshwa wa 38 kimataifa, wameaga Kombe la Dunia kwenye hatua ya makundi katika makala matatu yaliyopita. Walikutana na Ufaransa mnamo 2018 na kupokezwa kichapo cha 2-1. Hiyo ilikuwa mara ya nne kwa Ufaransa kuwapepeta kutokana na michuano mitano.

Tangu wakomoe Croatia 4-2 na kutawazwa wafalme wa dunia nchini Urusi mnamo 2018, Ufaransa wamejizolea taji jingine – UEFA Nations League – walilolitwaa Oktoba 2021 baada ya kupepeta Uhispania 2-1 kwenye fainali ya mashindano hayo mapya.

Hata hivyo, makali ya masogora hao wa kocha Didier Deschamps yameonekana kudidimia baada ya kubanduliwa katika hatua ya 16-bora ya Euro 2020 na kutoridhisha kwenye makala ya Nations League mwaka huu. Aidha, wameshinda mechi moja pekee kati ya sita zilizopita – 2-0 dhidi ya Austria mnamo Septemba.

Sasa wana presha ya kutorejesha kumbukumbu za mwaka wa 2002 ambapo waliweka rekodi duni ya kuwa mabingwa watetezi walioaga fainali za Kombe la Dunia katika hatua ya makundi bila ushindi wowote.

Kabla ya Ufaransa, mabingwa wote wengine watetezi wa Kombe la Dunia – Ujerumani (2014), Uhispania (2010) na Italia (2006) – waliaga makala yaliyofuata ya kipute hicho kwenye hatua ya makundi. Ni Brazil pekee mnamo 2006 waliowahi kushinda mchuano wa kwanza wa Kombe la Dunia wakiwa mabingwa watetezi.

Baada ya kukwaruzana na Australia, Ufaransa wataonana na Denmark (Novemba 26) kisha Tunisia (Novemba 30). Deschamps aliyetarajiwa kuita fowadi wa Manchester United, Anthony Martial, kujaza nafasi ya Benzema kambini mwake, amesema hana mpango wa kufanya hivyo.

Nafasi ya Kimpembe ilichukuliwa na Axel Disasi huku Randal Kolo Muani akijaza pengo la Nkunku. Beki Raphael Varane aliyekosa mechi tano zilizopita za Manchester United, bado hajapona kabisa jeraha la paja na huenda akakosa kupangwa katika kikosi cha kwanza cha Ufaransa dhidi ya Australia.

“Licha ya visa vingi vya majeraha, tutajitahidi kadri ya uwezo kukabiliana na kibarua kizito kinachotusubiri,” akasema Deschamps aliyeongoza Ufaransa kukomoa Brazil 3-0 kwenye fainali za Kombe la Dunia 1998 akivalia utepe wa nahodha.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Gareth Bale aongoza Wales...

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Argentina roho juu wakishuka...

T L