• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:22 PM
Arjen Robben astaafu kwenye ulingo wa soka kwa mara nyingine

Arjen Robben astaafu kwenye ulingo wa soka kwa mara nyingine

Na MASHIRIKA

KIGOGO Arjen Robben amestaafu kwenye ulingo wa soka kwa mara ya pili akiwa na umri wa miaka 37.

Nyota huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Uholanzi aliangika daluga zake kwenye ulingo wa soka kwa mara ya kwanza mnamo 2019 kabla ya kubatilisha maamuzi hayo na kurejea katika kikosi chake za zamani cha Groningen alichokichezea hadi mwisho wa msimu wa 2020-21.

Wepesi wa kupata majeraha mabaya pamoja na janga la corona katika msimu wake wa pili kambini mwa Groningen ni kiini cha Robben kutangaza kustaafu tena.

Akivalia jezi za Chelsea, Robben aliwahi kuongoza kikosi hicho kuzoa mataji mawili ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), mawili ya League Cup na Kombe la FA.

Aliwahi pia kuchezea PSV Eindhoven, Real Madrid na Bayern Munich. Robben alichezea Uholanzi mara 96 na akafunga jumla ya mabao 37.

“Nimeamua kutamatisha kipindi changu cha kucheza soka japo maamuzi yenyewe yalikuwa magumu. Namshukuru kila mmoja aliyeniunga mkono wakati wote nikiwa uwanjani,” akasema Robben.

Baada ya kusajiliwa na kocha Claudio Ranieri kabla ya kupigwa kalamu na Chelsea mnamo 2004, Robben alikuwa tegemeo kubwa kambini mwa kikosi hicho alichokisaidia kutwaa mataji ya EPL mnamo 2004-05 na 2005-06.

Alisajiliwa na Real Madrid mnamo 2007 na akashindia kikosi hicho ubingwa wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) katika msimu wake wa kwanza.

Aliingia katika sajili rasmi ya Bayern Munich mnamo 2009 na akasaidia kikosi hicho kutia kapuni mataji matatu kwa mpigo mnamo 2013 huku akifunga bao dhidi ya Borussia Dortmund na kuvunia miamba hao ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) uwanjani Wembley, Uingereza. Hadi alipotangaza kustaafu kwa mara ya kwanza, Robben alikuwa mchezaji wa Bayern.

Alikuwa sehemu ya kikosi cha Uholanzi kilichoshindwa na Uhispania kwenye fainali ya Kombe la Dunia mnamo 2010 nchini Afrika Kusini. Alistaafu soka ya kimataifa mnamo 2017 baada ya Uholanzi kushindwa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia zilizoandaliwa nchini Urusi mnamo 2018.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

TAHARIRI: Sekta ya uchukuzi ikombolewe sasa

PSG wamsajili kipa Gianluigi Donnarumma wa Italia bila ada...