• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 4:54 PM
Arsenal wakomoa Man-United uwanjani Emirates na kuendeleza ubabe wao katika EPL msimu huu

Arsenal wakomoa Man-United uwanjani Emirates na kuendeleza ubabe wao katika EPL msimu huu

Na MASHIRIKA

ARSENAL waliendelea kudhibiti kilele cha jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya bao la dakika ya mwisho kutoka kwa fowadi Eddie Nketiah kuwapa ushindi muhimu wa 3-2 dhidi ya Manchester United uwanjani Emirates.

Arsenal walishuka dimbani wakiwa na presha ya kudumisha pengo la alama tano kati yao na nambari mbili Manchester City baada ya mabingwa hao watetezi kucharaza Wolverhampton Wanderers 3-0 katika pambano la awali la EPL.

Vijana hao wa kocha Mikel Arteta walicheza kwa kujiamini licha ya kujipata chini katika dakika ya 17 baada ya Marcus Rashford kuvurumisha kombora lililoacha hoi kipa Aaron Ramsdale.

Arsenal walisawazisha mambo dakika saba baadaye kupitia Nketiah aliyekamilisha krosi ya Granit Xhaka. Ingawa Bukayo Saka aliwaweka Arsenal uongozini dakika nane baada ya kipindi cha pili kurejelewa, juhudi zake zilifutwa na Lisandro Martinez aliyefunga bao lake la kwanza kambini mwa Man-United.

Badala ya kutamauka, Arsenal walikita kambi langoni mwa wageni wao na nusura wafunge mabao mawili ya haraka kupitia Saka aliyeshuhudia fataki yake ikigonga mhimili wa lango na Nketiah aliyemwajibisha vilivyo kipa David de Gea.

Presha hiyo kutoka kwa Arsenal ilizaa matunda mwishowe baada ya Nketiah kucheka na nyavu na hivyo kuendeleza msururu wa matokeo bora tangu aaminiwe kujaza nafasi ya Gabriel Jesus anayeuguza jeraha la goti.

Arsenal sasa wanaselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 50 baada ya mechi 19. Man-United wanakamata nafasi ya nne kwa alama 39 sawa na Newcastle United. Arsenal walishuka ugani Emirates wakilenga kulipiza kisasi dhidi ya mabingwa mara 20 wa EPL – kikosi cha pekee ambacho kimewatandika ligini kufikia sasa msimu huu.

Tofauti na Man-United walioambulia sare ya 1-1 dhidi ya Crystal Palace katika pambano lao la awali la EPL, Arsenal walikuwa na kiu ya kuendeleza ubabe uliowavunia ushindi muhimu wa 2-0 dhidi ya Tottenham Hotspur ugenini mnamo Januari 15, 2022.

Alama 50 zinazojivunia na Arsenal kufikia nusu ya kampeni ya EPL muhula huu zinaweka hai ndoto ya kufikia rekodi ya Man-City waliotawazwa wafalme wa Uingereza mnamo 2017-18 baada ya kujizolea jumla ya pointi 100.

Arsenal, ambao hawajapoteza mchuano wowote kati ya 13 zilizopita katika EPL, wameshinda mechi 11 kati ya hizo. Hata hivyo, hawajawahi kukamilisha kampeni ya EPL ndani ya mduara wa nne-bora tangu 2016 na wanawania sasa ubingwa wa kipute hicho kwa mara ya 14 katika historia na mara ya kwanza tangu 2003-04.

Ingawa Newcastle United walikomesha rekodi yao ya kushinda mechi 10 mfululizo kwa sare tasa mwanzoni mwa Januari 2023 ugani Emirates, Arsenal walipigwa 3-1 na Man-United katika mkondo wa kwanza wa EPL msimu huu ugani Old Trafford.

Bao la Saka dhidi ya Man-United lilimfanya kuwa mchezaji wa tatu wa Arsenal kuwahi kufunga Man-United katika mechi tatu mfululizo za EPL baada ya Freddie Ljungberg na Thierry Henry.

MATOKEO YA EPL (Jumamosi):

Leeds 0-0 Brentford

Man-City 3-0 Wolves

Arsenal 3-2 Man-United

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Wafugaji Lamu wahofia kutofaidi kwa mauzo ya mifugo nje ya...

Nakuru City Queens wanyorosha Ulinzi Starlets, Zetech...

T L