• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Arsenal wazamisha chombo cha Spurs ligini

Arsenal wazamisha chombo cha Spurs ligini

Na MASHIRIKA

UFUFUO wa makali ya Arsenal chini ya kocha Mikel Arteta ulidhihirika wikendi baada ya mabingwa hao mara 13 wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kuwacharaza mahasimu wao wa London Kaskazini, Tottenham Hotspur, 3-1 ugani Emirates.

Arsenal walivuta mkia wa jedwali baada ya kupoteza mechi tatu za ufunguzi wa muhula huu dhidi ya Brentford, Chelsea na mabingwa watetezi Manchester City. Wakati huo, Spurs walikuwa wakidhibiti kilele cha jedwali la EPL chini ya mkufunzi Nuno Espirito aliyetokea Wolves kujaza pengo la Jose Mourinho mwishoni mwa msimu jana wa 2020-21.

Hata hivyo, Arsenal waliendeleza masaibu ya Spurs ambao walifutiwa machozi na Son Heung-Min katika dakika ya 79 baada ya Arsenal kufunga mabao matatu katika kipindi cha kwanza kupitia Emile Smith Rowe, Pierre-Emerick Aubameyang na Bukayo Saka aliyeshirikiana vilivyo na Smith Rowe pamoja na Martin Odegaard.

Chini ya kocha Mikel Arteta, Arsenal walishuka dimbani wakipania kuendeleza ubabe uliowavunia ushindi wa 3-0 dhidi ya AFC Wimbledon katika Carabao Cup mnamo Jumatano uwanjani Emirates.

Kwa upande wao, Spurs walikuwa wakilenga kujinyanyua baada ya kujipata katika ulazima wa kutegemea mikwaju ya penalti ili kubwaga Wolverhampton Wanderers kwenye Carabao Cup baada ya sare ya 2-2 ugani Molineux.

Katika kampeni za msimu uliopita wa 2020-21, Arsenal walisajili ushindi wa 2-1 dhidi ya Spurs katika mkondo wa pili wa debi ya London baada ya Spurs waliokuwa chini ya Mourinho kuwazamisha 2-0 katika mchuano wa mkondo wa kwanza.

Kubwa zaidi lililofanya mashabiki kupigia upatu masogora wa Arteta kutamba katika gozi hilo la London Kasakazini ni rekodi nzuri wanayojivunia dhidi ya Spurs ambao walikuwa wameshinda mechi moja pekee ya EPL kati ya 28 za awali dhidi ya Arsenal ugenini.

Baada ya kupoteza mechi tatu za ufunguzi wa kampeni za EPL msimu huu, Arsenal walipiga Norwich City 1-0 ligini mnamo Septemba 11 kabla ya kusajili matokeo sawa na hayo siku saba baadaye.

Ingawa safu ya mbele ya Arsenal ilikuwa butu katika michuano iliyopita mwanzoni mwa msimu huu, miamba hao hawajawahi kushindwa kufunga bao dhidi ya Spurs ligini tangu mwaka wa 2000.

Kinyume na Arsenal waliopoteza mechi tatu mfululizo za ufunguzi wa EPL msimu huu bila kufunga bao lolote, Spurs walifungua kampeni zao kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Man-City, Wolves na Watford mfululizo. Hata hivyo, uthabiti wao ulitiwa kigezoni katika michuano miwili iliyopita ligini ambapo walipigwa 3-0 na Crystal Palace na Chelsea mtawalia kabla ya Arsenal pia kuwatandika.

Baada ya kivumbi dhidi ya Arsenal, Spurs watakuwa wenyeji wa NS Mura ya Slovenia katika mechi ya makundi ya UEFA Europa Conference League kabla ya kupimana ubabe na Aston Villa na Newcastle United ligini.

Arsenal wameratibiwa kumenyana na Brighton, Palace na Villa kwa usanjari huo.

  • Tags

You can share this post!

Kinoti akwepa hukumu

Muturi aahidi vijana makuu akichaguliwa rais