• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 1:12 PM
Muturi aahidi vijana makuu akichaguliwa rais

Muturi aahidi vijana makuu akichaguliwa rais

Na CHARLES WANYORO

Spika wa Bunge la Taifa, Justin Muturi, ameahidi kuteua vijana katika nyadhifa muhimu katika serikali yake iwapo atachaguliwa rais mwaka ujao, hatua ambayo alisema italeta ‘damu’ mpya katika serikali na kumaliza ufisadi.

Alisema viongozi wa sasa wameruhusu ufisadi kunawiri kwa hivyo hawafai kukubaliwa kushikilia nyadhifa muhimu ili nchi iweze kustawi.

Akihutubia viongozi wa mashinani kutoka eneobunge la Buuri katika hoteli ya Sera Park, Kaunti ya Meru, Bw Muturi alisema viongozi vijana walishikilia nyadhifa muhimu katika serikali ya Rais Jomo Kenyatta iliyoweka msingi wa nchi hii.

Alisema vijana wanafaa kuhimizwa kushikilia nyadhifa za uongozi kama mawaziri na makatibu wa wizara katika juhudi za kuwa na maono mapya na watu wasio na doa katika serikali.

Spika huyo aliongeza kuwa Kenya ingekuwa imepata ustawi wa viwanda iwapo viongozi walafi na fisadi hawangekuwa wakiteuliwa kushikilia nyadhifa muhimu na kupora pesa zinazotengewa maendeleo.

Alitoa mfano wa mradi wa unyunyiziaji maji wa Galana Kulalu aliosema umevurugwa na watu ambao wamekuwa serikalini kwa miaka mingi.

“Baadhi ya watu ambao wamekuwa serikalini kwa miaka mingi huwa wanafikiria wizi tu. Serikali yangu itakuwa ya vijana, wazee wanafaa kujiandaa kuondoka. Serikali ya kwanza ilisimamiwa na viongozi vijana kama Tom Mboya, Mwai Kibaki na wengine wengi na ni wakati huo ambao msingi wa nchi uliwekwa,” akasema Muturi.

“Ni Jomo Kenyatta na Jaramogi Oginga waliokuwa wazee. Tunataka watu wasio na doa,” alisema.B w Muturi alisema kwamba pesa nyingi hupotea kupitia ufisadi na nyingine zaidi Kwa kushtaki wanaohusika na uovu huo.

You can share this post!

Arsenal wazamisha chombo cha Spurs ligini

Musalia na Weta watakiwa kusahau urais na kumuunga mkono...