• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Atletico Madrid wapiga Real Valladolid na kutia kapuni ufalme wa La Liga

Atletico Madrid wapiga Real Valladolid na kutia kapuni ufalme wa La Liga

Na MASHIRIKA

ATLETICO Madrid waliwanyima Real Madrid fursa ya kuhifadhi ubingwa wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) baada ya kutoka nyuma na kuwapepeta Real Valladolid 2-1 katika mechi ya mwisho msimu huu.

Chini ya kocha Diego Simeone, Atletico walijipata chini katika dakika ya 18 baada ya Oscar Plano kufungia Valladolid kabla ya Angel Correa kusawazisha mambo katika dakika ya 57.

Nyota wa zamani wa Barcelona, Luis Suarez alizamisha kabisa chombo cha Valladolid katika dakika ya 67 na kuvunia Atletico taji lao la kwanza la La Liga tangu 2013-14.

Chini ya kocha Zinedine Zidane, Real pia walitoka nyuma na kuwapiga Villarreal 2-1. Hata hivyo, walikosa kutwaa taji kwa sababu walihitaji Atletico wapoteze alama ndipo wao watawazwe wafalme. Taji hilo lililonyanyuliwa na Atletico lilikuwa lao la kwanza chini ya kipindi cha miaka saba na la 11 kwa jumla.

Ushindi dhidi ya Valladolid uliwawezesha Atletico kukamilisha kampeni za La Liga msimu huu kwa alama 86, mbili zaidi kuliko Real Madrid waliokamilisha muhula bila ya taji lolote.

Baadhi ya mashabiki wa Atletico Madrid nje ya uwanja wa Jose Zorilla mjini Valladolid, Mei 22, 2021. Picha/ AFP

Bila ya kujivunia huduma za nahodha Lionel Messi, Barcelona waliwapiga Eibar 1-0 kupitia fowadi Antoine Griezmann. Messi alipewa na waajiri wake lilkizo ya mapema ili kujiandaa kwa fainali za Copa America zitakazoandaliwa na Argentina mwaka huu.

Ushindi huo ulidumisha Barcelona ya kocha Ronald Koeman katika nafasi ya tatu kwa alama 79, tano kuliko Sevilla waliofunga orodha ya nne-bora. Chini ya kocha Julen Lopetegui, Sevilla watapepetana na Alaves mnamo Mei 23, 2021.

Bao la Villarreal ambao kwa sasa wanajiandaa kwa fainali ya Europa League dhidi ya Manchester United mnamo Mei 26 lilifungwa na Yeremi Pino kabla ya Karim Benzema na Luka Modric kufungia Real.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Ruto aahidi kuepuka madeni akiwa rais

Muturi atawazwa msemaji Mlima Kenya