• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Atletico Madrid wasuka mpango wa kumsajili Ronaldo

Atletico Madrid wasuka mpango wa kumsajili Ronaldo

Na MASHIRIKA

ATLETICO Madrid wamefichua mpango wa kumtia fowadi Antoine Griezmann, 31, mnadani ili kufanikisha uhamisho wa Cristiano Ronaldo kutoka Manchester United hadi uwanjani Wanda Metropolitano.

Ronaldo, 37, ametaka Man-United wamwachilie kuondoka ugani Old Trafford baada ya mabingwa hao mara 20 wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kutofuzu kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Licha ya Ronaldo kuibuka mfungaji bora wa Red Devils katika EPL muhula uliopita kwa mabao 18, waajiri wake walitupwa katika nafasi ya sita jedwalini kwa alama 58 – idadi ndogo zaidi ya pointi katika historia yao tangu wajizolee alama 59 mnamo 1990-91.

Kusalia ugani Old Trafford kutashuhudia mshindi huyo mara tano wa Ballon d’Or, akinogesha ligi ndogo ya Europa League mnamo 2022-23 – kwa mara ya kwanza kabisa katika taaluma yake.

Ni jambo ambalo wakala Jorge Mendes amesema “litadunisha hadhi ya mteja wake ambaye sasa hana msukumo wa kuendelea kuvalia jezi za Red Devils”.

Kujiunga na Atletico kutampa Ronaldo fursa ya kutandaza soka ya UEFA ikizingatiwa kwamba kikosi hicho cha kocha Diego Simeone kiliambulia nafasi ya tatu msimu jana katika Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Kinyume na ilivyotarajiwa, Ronaldo hajapata ofa yoyote kutoka kwa vikosi vya haiba. Bayern Munich na Chelsea wamesema hawana mpango wa kusajili nahodha huyo wa timu ya taifa ya Ureno.

Kwa mujibu wa gazeti la The Times, Atletico hawataweza kumtwaa Ronaldo hadi watakapopunguza gharama ya matumizi yao ya fedha. Kizungumkuti ni kuwa mpango wao wa kushawishi Paris Saint-Germain (PSG) kusajili Griezmann kwa mkopo umegonga ukuta kutokana na matokeo duni ya Mfaransa huyo aliyefunga mabao matatu pekee ligini msimu jana.

Griezmann alisajiliwa na Barcelona kutoka Atletico kwa Sh14.6 bilioni miaka mitatu iliyopita. Alirejea jijini Madrid kwa mkopo wa miaka miwili mwishoni mwa 2020-21 huku Atletico wakiwa na ulazima wa kumsajili upya kwa Sh4.9 bilioni kufikia Juni 2023.

Ilivyo, Atletico hawawezi kumdumishwa Griezmann ugani Wanda Metropolitano kwa ujira wa Sh50 milioni kwa wiki huku wakimlipa pia Ronaldo zaidi ya Sh68 milioni kwa juma.

Diego atakuwa mwepesi wa kusajili Ronaldo aliyefungia Man-United mabao 24 katika mashindano yote msimu jana. Hakuna sogora wa Atletico alifunga zaidi ya mabao 13 mnamo 2021-22.

Hata hivyo, huenda akapokelewa upya nchini Uhispania kwa mseto wa hisia ikizingatiwa kuwa ni mwanasoka nguli wa Real Madrid ambao ni watani wakuu wa Atletico. Akiwa Real, Ronaldo aliweka rekodi ya kupachika wavuni mabao 450 katika kipindi cha miaka tisa.

Ingawa Man-United wana kiu ya kudumisha Ronaldo, kuondoka kwake huenda kukamvunia afueni Erik ten Hag – kocha wa tano kupokezwa mkataba wa kudumu ugani Old Trafford baada ya David Moyes, Louis van Gaal, Jose Mourinho na Ole Gunnar Solskjaer tangu Sir Alex Ferguson astaafu mnamo 2013.

Ronaldo aliwahi kuzozana na beki Harry Maguire kuhusu unahodha wa Man-United huku akikosoa mbinu za ukufunzi za Ralf Rangnick aliyetaka ashambulie zaidi katika mfumo mpya wa 4-3-3 uliokosa kuzaa matunda.

Kubanduka kwake kutapunguza pia gharama ya matumizi ya fedha ya Man-United na kumpa Ten Hag fursa ya kujishughulisha zaidi katika soko la uhamisho wa wachezaji na kukisuka upya kikosi chake.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Jaji na wakazi wa Kalimbini watishiwa kufukuzwa kutoka kwa...

Raila akataa kushiriki mdahalo wa urais

T L