• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Raila akataa kushiriki mdahalo wa urais

Raila akataa kushiriki mdahalo wa urais

NA CHARLES WASONGA

MGOMBEA urais wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga amesema kuwa hatahudhuria mdahalo wa urais kati yake na mgombea urais wa Kenya Kwanza William Ruto Jumanne jioni.

Badala yake Bw Odinga na mgombea mwenza wake Martha Karua watakuwa katika ukumbi wa kijamii wa Kaloleni, Nairobi kujibu masuala kutoka kwa wananchi kuhusu changamoto zinazowakumba.

Kwenye taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari Jumapili, Julai 24, 2022, Msemaji wa kampeni za Bw Odinga Makau Mutua, Bw Odinga alisema alifikia uamuzi huo baada ya Kenya Kwanza kusisitiza kuwa mdahalo huo haufai kuhusisha masuala ya ufisadi, maadili na uongozi bora.

“Kwa sababu mgombea urais wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) amesisitiza kuwa mdahalo huo haufai kuangazia masuala ya ufisadi, maadili na uongozi bora, mgombea wetu wa urais Raila Odinga haoni haja ya kushiriki. Hii ni kwa sababu masuala haya ndio nguzo kuu ya kampeni za Azimio,” akasema Profesa Mutua.

“Mdahalo wowote ambao hautaguzia masuala haya ambayo ndio chanzo cha madhila yanayowasibu raia wakati huu itakuwa ni sawa na dharau kwa Wakenya,” akaongeza.

Profesa Mutua alisema kuwa kwa kukubali kushiriki mdahalo ambako masuala hayo ya maadili hayatajadiliwa, Bw Odinga atakuwa akijipata akiendeleza kampeni za Dkt Ruto.

“Inakuwa kosa kubwa kumtunuku mtu kama huyo (Ruto) kwa kushiriki mdahalo kwenye jukwaa moja pamoja naye. Hatatusaidia kampeni zake ambazo zinaporomoka. Anaweza kujieleza kivyake na rekodi yake mbaya kwa wapigakura bila usaidizi wetu,” Profesa Mutua akasema.

“Badala yake tunapanga kushiriki katika kipindi ambacho kitapeperushwa kupitia runinga ambako tutajibu maswali kutoka kwa wananchi wa kawaida katika ukumbi wa kijamii wa Jericho, Mashariki mwa jiji la Nairobi,” akaongeza katia taarifa hiyo.

Mnamo msemaji wa kampeni za Dkt Ruto Hussein Mohamed alisema kuwa Naibu huyo wa Rais atashiriki mdahalo tu iwapo waandalizi watatoa muda mwingi kwa mjadala kuhusu masuala ya afya, uchumi, nyumba na gharama ya maisha.

“Mgombea urais wa Kenya Kwanza atashiriki mdahalo huo tu iwapo wasimamizi watatoa muda tosha kwa mjadala kuhusu uchumi, huduma za afya, nyumba, kando na masuala ya maadili na ufisadi,” akasema Bw Mohamed.

Mdahalo huo umeratibiwa kufanyika Jumanne, Julai 25, 2022, kuanzia saa mbili za usiku katika Chuo Kikuu cha Katoliki Afrika Mashariki (CUEA), mtaani Karen, Nairobi.

Utaendeshwa kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza itaanza saa kumi na moja na nusu jioni na kushirikisha mgombea urais wa chama cha Roots Profesa George Wajackoyah na mwenzake wa chama cha Agano David Mwaure Waihiga.

Awamu ya pili ya mdahalo huo imeratibiwa kuanza saa mbili za usiku na kushirikisha Dkt Ruto na Bw Odinga.

  • Tags

You can share this post!

Atletico Madrid wasuka mpango wa kumsajili Ronaldo

Edna Talava alenga makuu katika uigizaji

T L