• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Aubameyang apokonywa utepe wa unahodha kambini mwa Arsenal

Aubameyang apokonywa utepe wa unahodha kambini mwa Arsenal

Na MASHIRIKA

FOWADI Pierre-Emerick Aubameyang amepokonywa utepe wa unahodha kambini mwa Arsenal kutokana na utovu wa nidhamu.

Mshambuliaji huyo raia wa Gabon alitemwa katika kikosi kilichopepeta Southampton 3-0 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Disemba 11 na hatakuwa sehemu ya kikosi kitakachotegemewa na kocha Mikel Arteta dhidi ya West Ham United ligini mnamo Disemba 15, 2021.

“Tunatarajia wachezaji wetu wote, hasa nahodha wetu, kutii sheria zinazotudhibiti pamoja na kwa viwango vya juu tulivyowawekea na kukubaliana kama klabu,” ikasema sehemu ya taarifa ya Arsenal.

Aubameyang aliwahi pia kudondoshwa kwenye kikosi cha Arsenal kwa utovu wa nidhamu mnamo Machi 2021.

Wakati huo, alikosa kuwa sehemu ya timu iliyosajili ushindi wa 3-1 dhidi ya watani wao wakuu, Tottenham Hotspur.

Ingawa Arteta hajafichua kilichofanywa na Aubameyang mara hii, gazeti la The Athletic nchini Uingereza limeshikilia kwamba mvamizi huyo wa zamani wa Borussia Dortmund alichelewa kurejea kambini kutoka safari ya ng’ambo ambayo haikuwa imeidhinishwa.

“Tumekuwa wazi kila mara. Tuna kanuni ambazo zinastahili kuongoza kila mmoja wetu kikosini. Siwezi kufichua kila kitu kilichotokea katika chumba cha kubadilishia sare,” akasema Arteta baada ya mechi dhidi ya Southampton.

Aubameyang aliyejiunga na Arsenal mnamo 2018 kutoka Dortmund ya Ujerumani kwa Sh8.7 bilioni, alitia saini mkataba mpya wa miaka mitatu mnamo 2020.

Kufikia sasa msimu huu, amefunga mabao manne pekee kutokana na mechi 14 na hajatikisa nyavu za wapinzani tangu Oktoba 22, 2021.

Arsenal wanashikilia nafasi ya sita jedwalini kwa alama 26 huku pengo la pointi 12 likitamalaki kati yao na viongozi Manchester City ambao pia ni mabingwa watetezi.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Smalling aongoza AS Roma kutandika Spezia katika Serie A

TUK Hummer mabingwa Grandpa Super Cup

T L