• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Baada ya sare na Gor Mahia sasa Bandari FC yapania kuichapa City Stars

Baada ya sare na Gor Mahia sasa Bandari FC yapania kuichapa City Stars

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

BAADA ya kutoka sare ya kutofungana na Gor Mahia jijini Nairobi sasa Bandari FC imepania kuhakikisha inazoa pointi zote tatu za Ligi Kuu ya FKF BetKing itakapokutana na City Stars FC katika uwanja wa Mbaraki Sports Club, Jumapili, Julai 4, 2021.

Meneja wa timu hiyo, Alber Ogari alisema walirudi Mombasa, Jumatano na kufanya mazoezi siku tatu kujitayarisha kwa mechi yao na City Stars hapo Jumapili ambapo wana tamaa kubwa ya kupata ushindi.

“Tulipocheza ugenini dhidi ya Gor, tulipoteza nafasi nyingi za kufunga lakini nina imani vijana wetu watapata alama zote tatu Jumapili. Kocha Andre Cassa Mbungo atafanyia kazi safu ya ushambulizi kusudi mastraika wetu watumie nafasi za kufunga tupate ushindi,” akasema Ogari.

Alisema wanataka kuwafurahisha mashabiki wao kwa kuwapatia matokeo mazuri.

“Tunaamini tutawafurahisha mashabiki wetu ambao tunahitaji wasikie tumeishinda City Stars na tupate kuwa sehemu nzuri katika jedwali la ligi,” akasema.

Ogari amesema watamuangalia straika wao Yema Mwana ambaye alikuwa ameumia na hakuwako Nairobi kwa mechi ya Gor.

“Nina matumaini Mwana amepona na tutamuangalia mazoezini kama yuko sawa ili kocha Mbungo afikirie kama atamchezesha,” akasema.

Alieleza kuwa wakati wa mechi na Gor, beki Atariza Amai aliumia kichwa aliporukia mpira wa juu na kugongana na mchezaji wa Gor lakini anaendelea vizuri na huenda akawa sawa kwani hata wakati wa mechi hiyo, aliendelea kucheza hadi mwisho.

Mwana alionekana akifanya mazoezi na wachezaji wa timu ya Bandari Youth katika uwanja wa Mbaraki Sports Club siku za Jumatano na Alhamisi akiwa pamoja na Shaaban Kenga ambaye amekuwa nje kwa miezi kadhaa kutokana na kuvunjika mguu.

You can share this post!

Viongozi wa Kiislamu washutumu TSC kutoajiri walimu wengi...

Sergio Ramos akubali kuchezea PSG kwa mkataba wa miaka...